Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Septemba 2023

14:21:48
1392987

Kuendelea kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na siasa za kindumakuwili za Magharibi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani amezungumzia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi mdogo wa Uturuki mjini New York na kubainisha kwamba, kudharau vitabu vitakatifu ni jambo la kuchukiza.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashaur ya Kigeni ya Marekani anasema hayo katika hali ambayo, ameeleza kwamba, Washington inaunga mkono uhuru wa kujieleza kama kipengele cha msingi cha demokrasia yoyote na iliyobainishwa katika Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani."

Msimamo huu umechukuliwa katika kujibu kuvunjiwa heshima tena Qur'an Tukufu. Siku chache zilizopita, mtu mmoja aliivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya Ubalozi mdogo wa Uturuki mjini New York, kwa kukitupa chini kitabu kitakatifu cha Waislamu na kukivunjia heshima kwa kukikanyaga.

Maafisa usalama wa ubalozi mdogo wa Uturuki waliingilia kati baada ya tukio hili na kumuondoa mtu aliyetajwa mahali hapo. Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Ulaya hususan eneo la Skandinavia zimekuwa uwanja wa kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu

Tangu mwanzoni mwa majira ya kiangazi ya mwaka huu, kuvunjiwa heshima kwa Qur'ani Tukufu kwa njia ya uchomaji Qur'ani kumetokea mara nyingi katika nchi mbili za kaskazini mwa Ulaya, yaani Sweden na Denmark, na baadhi ya watu wenye chuki dhidi ya Uislamu, kama vile Momika Salwan pamoja na wanachama wa vyama vya mrengo wa kulia wamejitokeza hadharani mara kadhaa na kukivunjia heshima kitabu hiki kitakatifu. Chini ya usaidizi wa polisi wa Uswidi na Denmark, watu hawa walichoma moto Qur'ani Tukufu na maandamano ya Waislamu pia yalizimwa na kukandamizwa na polisi.

Kuvunjiwa heshima kwa Qur'ani Tukufu kumekabiliwa na wimbi la malalamiko makubwa hususan katika ulimwengu wa Kiislamu na kupelekea maandamano makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na nchi nyinginezo.

Kuhusiana na hilo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mwezi uliopita ilizitaka nchi wanachama wake kuchukua hatua zinazofaa za kisiasa na kiuchumi dhidi ya Uswidi na nchi nyinginezo ambazo zinaruhusu kuchomwa moto vitabu vitakatifu vya Kiislamu. Mapema Julai 2023, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lililaani kuvunjiwa heshima Qur'ani na zikapasisha azimio lililopendekezwa na nchi za Kiislamu na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kuchunguza suala hili na kutoa ripoti.

Licha ya kuwepo kwa radiamali kubwa ya Waislamu na nchi za Kiislamu kuhusu suala la Qur'ani kuchomwa moto katika nchi mbili za kaskazini mwa Ulaya, yaani Sweden na Denmark, na upinzani wa wazi wa Umoja wa Mataifa dhidi ya kitendo hiki cha dharau na kisichokubalika na hata ahadi za mamlaka za nchi hizi mbili za kuzuia vitendo hivyo, lakini watu wenye chuki dhidi ya Uislamu wameendelea kuvunjia heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa uhuru na himaya kamili ya vyombo vya usalama. Filihali kitendo hiki kiovu kimechukua wigo mpana na kuenea hadi Marekani.

Licha ya radiamali kali za Waislamu, mataifa ya Kiislamu na hata Umoja wa Mataifa dhidi ya mamluki wa Uzayuni kama Momika Salwan ambaye mfungamano wake na Tel Aviv ni jambo lisilo na shaka, lakini mataifa ya Magharibi yangali yanatoa idhini kwa watu wenye chuki na Uislamu kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu hususan kuchomwa moto Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni.

Himaya na uungaji mkono wa Wamagharibi kwa kitendo cha kuvunjiwa heshima na cha kuchomwa moto Qur'ani unafanyika katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa unapinga kitendo hicho cha aibu. Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema: Miguel Moratinos, Mkuu wa Asasi ya Staarabu ya Umoja wa Mataifa amelaani vikali kuchomwa moto Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti mmoja katikati ya mji wa Stockholm, Sweden.

Inaonekana kuwa, Wamagharibi wanapuuza kwa makusudi tofauti baina ya uhuru wa kusema na kutusi matukufu ya dini. Tukitupia jicho vigezo vya kindumakuwili vya madola Magharibi zikiwemo Sweden na Denmark kuhusiana na uhuru wa kutoa maoni tunaona kuwa, jambo hili hubeba maana pale tu linapohoji na kuvunjia heshhima jambo ambalo ndio mtazamo wa Magharibi kama vile chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu. Lakini mambo ni kinyume kabisa kuhusiana na masuala mengine kama ngano ya Holocaust.

Mfano mwingine wa wazi ni vita vya Ukraine na Russia ambapo wanaotoa maoni na mitazamo kuhusu vita hivyo ambayo ni kinyume na matazmo wa madola ya Magharibi hukabuiliwa na mashinikizo ya kila upande na wakati mwingine kukabiliwa na mashtaka kama ilivyo katika suala la Holocaust.

342/