Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Septemba 2023

14:26:28
1392994

Gabon yatangaza kipindi cha mpito cha miaka 2 kabla ya uchaguzi

Serikali ya kijeshi ya Gabon imetangaza kipindi cha mpito cha miaka miwili kabla ya kuitishwa uchaguzi mkuu mwingine.

Serikali hiyo ya kijeshi ambayo ilinyakua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi Agosti 30, imesema kupitia Waziri Mkuu, Raymond Ndong Sima kuwa, wana hamu ya kuona utawala wa mpito unafikia tamati katika kipindi cha miezi 24 ijayo.

Sima amesema uamuzi wa kutangaza kipindi cha mpito cha miaka miwili kabla ya kuitishwa uchaguzi mkuu mwingine una mantiki. 

Aidha amesema kwa mujibu wa hati ya mpito, hakuna kiongozi wa serikali hiyo ya muda atakayeruhusiwa kugombea urais katika uchaguzi ujao nchini humo.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa serikali ya mpito ya Gabon amebanisha kuwa, hakuna kitu kinamchomzuia kiongozi wa mapinduzi nchini humo kugombea urais. 

Jenerali Brice Oligui Nguema, ambaye aliapishwa kama rais wa muda Jumatatu iliyopita, ameahidi kuendesha uchaguzi huru, wa wazi na wa kuaminika ili kurejesha utawala wa kiraia nchini Gabon.

Sima, ambaye ni mchumi mwenye umri wa miaka 68, alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ali Bongo, ambaye aliondolewa madarakani na maafisa wa kijeshi mnamo Agosti 30.

Amesema katika matamshi hayo ya jana Jumapili kuwa, serikali hiyo ya mpito ni jumuishi, na kwa msingi huo hivi sasa hakuna upinzani wala mrengo wa walio wengi serikalini. 

 342/