Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

14 Septemba 2023

11:46:35
1393668

Sarkozy: Kupewa uanachama wa NATO Ukraine ni kutasababisha vita vya dunia

Rais wa zamani wa Ufaransa amesema kuwa, Ukraine haipaswi kuruhusiwa kujiunga na NATO kwa namna yoyote ile kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kupelekea kuzuka vita vya dunia.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo likimnukuu Nicolas Sarkozy akionya kuhusu hatari za kutanua vita nchini Ukraine na uwezekano wa kuzuka vita vingine vya dunia iwapo nchi za Magharibi zitaruhusu Ukraine kujiunga na NATO.

Rais huyo wa zamani wa Ufaransa amesema, Russia inalichukulia suala la kujiunga Ukraine na NATO kuwa ni sawa na kutangaza vita vya moja kwa moja vya nchi za Magharibi dhidi yake na hilo linaweza kusababisha kuenea vita dunia nzima.

Amesema, ni wazi kwamba nchi za Magharibi haziwezi kuiangamiza Russia kwani ni dola kubwa lenye nguvu za kijeshi na ni la pili kwa nguvu za nyuklia duniani hata tukiburuzwa kwenye vita vya dunia.Sarkozy pia amewashangaa wanasiasa wa nchi za Magharibi wanaodai kuwa Putin si mtu wa kuzungumza naye wakati hawajawahi kuonana naye hata mara moja.

Ikumbukwe kwamba jeshi la Russia lilianzisha "operesheni yake maalumu ya kijeshi" mashariki mwa Ukraine tarehe 24 Februari 2022. 

Marekani na nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vingi Moscow kwa kisingizio cha vita vya Ukraine lakini hadi hivi sasa ni nchi za Ulaya ndizo zinazopata hasara kubwa zaidi kwa vikwazo zilivyoiwekea Russia. 

Katika upande mwingine, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, amesema kuwa, shehena na msafara wowote wa silaha za kijeshi unaopelekwa Ukraine ni shabaha halali ya mashambulizi ya vikosi vya ulinzi vya Russia.

342/