Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

14 Septemba 2023

11:48:32
1393670

Njama mpya za Marekani za kushadidisha vita vya Ukraine

Viongozi wa Marekani wametangaza kuwa, serikali ya Joe Biden imekaribia kupasisha muswada wa kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kubeba mabomu ya vishada.

Wakuu hao wa Marekani wanadai kuwa, mabomu ya vishada waliyoipa Ukraine huko nyuma yamezaa matunda na hivi sasa wanafikiria kuipa serikali ya Kyiv mfumo wa makombora wa ATACMS au ule wa kufyatulia matoketi wa GMLRS au mifumo yote miwili kwa pamoja.

Makombora ya ATACMS yana uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 320 huku maroketi ya GMLRS yakiwa na uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 72 na yana uwezo wa kubeba mabomu ya vishada. Mfumo wa makombora wa ATACMS una uwezo wa kubeba zaidi ya mabomu 300 madogomadogo huku maroketi ya GMLRS yakiwa na uwezo wa kubeba mabomu hata 404 madogomadogo kwa wakati mmoja. Viongozi wa Marekani wanadai kuwa, vita vya “kujibu mashambulizi” vya Ukraine ndio kwanza vimeanza hivyo White House inataka kukitumia vizuri kipindi hiki hassas na muhimu mno kwake katika vita dhidi ya Russia. Kwa muda wa miezi mingi sasa Marekani inafikiria kuipa Ukraine mifumo hiyo ya makombora lakini inaogopa kwani ikifanya hivyo itakuwa ni kutangaza vita moja kwa moja na Russia. Makombora ya ATACMS yenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomia 320 yana uwezo mara nne zaidi ya makombora iliyopewa serikali ya Ukraine huko nyuma na Marekani. Kabla ya hapo pia viongozi wa Washington waliipa serikali ya vibaraka wao ya Kyiv mabomu ya vishada pamoja na risasi zenye urani iliyokhafifishwa, hatua ambazo zililalamikiwa vikali duniani.Katika upande mwingine na sambamba na kupamba moto vita baina ya Russia na Ukraine, kundi moja la wabunge wa Marekani kutoka vyama vyote viwili vya Democrats na Republicans limemwandikia barua Joe Biden na kumtaka aipe serikali ya Ukraine silaha kali zaidi. Kundi hilo la wabunge wanne wa Republican na Democrats huko Marekani limedai kuwa, serikali ya Kyiv inahitaji makombora ya kupiga masafa marefu zaidi. Hadi sasa Marekani inaogopa kuipa Ukraine makombora hayo kwa sababu haijui Russia italipokea kwa hasira kiasi gani jambo hilo. Mara kwa mara viongozi wa Marekani wanadai kuwa silaha wanazoipa Ukraine hazikusudiwi kushambulia ardhi ya Russia lakini kitendo cha Marekani cha kuamua kuipa Ukraine makombora ya ATACMS na maroketi ya GMLRS ni ushahidi wa wazi kuwa viongozi wa Ikulu ya Marekani, White House, ndio wanaopigana vita na Russia kwa jina la Ukraine na hawana nia kabisa ya kupunguza makali ya vita hivyo. Viongozi wa Ukraine lakini wanashinikiza muda wote wapewe makombora ya masafa marefu zaidi na nchi za Magharibi ikiwemo Ujerumani. Hivi karibuni waziri wa mambo ya nje wa Ukraine wakati alipoonana na waziri mwenzake wa Ujerumani, alishinikiza pia ipewe Kyiv makombora aina ya Taurus yenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 500 lakini Ujerumani haioneshi nia ya kufanya hivyo. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani amekataa waziwazi mashinikizo hayo ya Kyiv na kusema kuwa, hakuna ulazima wowote kwa nchi yake kuifuata Marekani katika kuipa makombora ya masafa marefu Ukraine. Kabla ya hapo nchi za Ulaya za Uingereza na Ufaransa ziliipa Ukraine makombora ya cruise ambayo yanafanana na yale ya Taurus ya Ujerumani.Serikali ya Marekani inaamini kuwa, kama Russia itashinda vita vya Ukraine licha ya misaada yote iliyopewa serikali ya Kyiv itakuwa ni pigo kubwa wa jeshi la nchi za Magharibi NATO na utaongezeka mno ushawishi wa Russia kimataifa. Hata mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya pia utabadilika kwa madhara ya madola ya Magharibi. Hivyo Washington imeamua kurefusha vita vya Ukraine ikiwa ni pamoja na kuipa Kyiv silaha za kila namna kujaribu kuzuia ushindi wa Russia. Aidha rais wa Marekani, Joe Biden na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na kiusalama wa serikalli yake wanaamini kuwa, vita vya Ukraine ni fursa ya kipekee kwao na ambayo si rahisi kupatikana tena katika kuidhoofisha Russia na hatimaye kuzuia kuundika mfumo wa kambi kadhaa duniani. Viongozi wa Marekani hawajali ni roho ngapi za watu zitapotea na ni uharibifu na maangamizi kiasi gani itapata Ukraine na watu wake.

342/