Main Title

source : Parstoday
Jumapili

17 Septemba 2023

19:27:15
1394174

Akthari ya vijana Uingereza wanafikiria kuhama wanakoishi ili kuhangaikia fursa

Utafiti uliofanywa nchini Uingereza umegundua kwamba Waingereza wengi wenye umri wa miaka 16 hadi 18 wanasema wanahitaji kuhama kutoka maeneo yao, ikiwa ni pamoja na yale ya kaskazini mashariki, Yorkshire na mashariki mwa Uingereza, kutokana na kukosa fursa za ajira na kujiendeleza.

Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Wakfu wa Uhamaji wa Kijamii (Social Mobility Foundation), kwa wastani zaidi ya 85% ya vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 18 wanahisi wanahitaji kuhama katika maeneo wanakoishi.

Idadi hiyo ilifikia 95% mashariki mwa Uingereza, 91% kaskazini mashariki, 90% huko Yorkshire na 88% kaskazini magharibi.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, watu wapatao 2,000 walishiriki katika uchunguzi huo wa maoni.

Tom Brennan kijana kutoka Ipswich anasema, "Kusema ukweli, jambo kubwa zaidi kwa mji huu ni ukaribu wake na London. Hakuna fursa nyingi au matukio ya maana yanayotokea hapa."Kijana huyo ameendelea kueleza: "hakuna fursa nyingi za sayansi ya kompyuta zinazopatikana hapa. Labda nitahamia London," na akaongezea kwa kusema  "nitaikosa familia yangu, lakini zaidi ya hayo hakuna mengi ambayo nitayakosa hapa Ipswich," amemalizia kueleza kijana huyo wa miaka 18 ambaye anataka awe mtaalamu wa programu za kompyuta.

Amina Rashid, anayeishi Preston, yeye amesema, "hakuna mengi hasa ya kufanya hapa. Kwa kweli hakuna chochote. Kwa kawaida mimi huenda katika miji mingine mikubwa kama vile Liverpool au Manchester kufanya mambo mbalimbali”.

Mashariki mwa Uingereza ni kitovu cha baadhi ya miji yenye hali duni nchini Uingereza kama vile Jaywick, ambao umetajwa kuwa eneo lenye watu wengi zaidi wenye hali duni na uhaba wa fursa na suhula nchini humo.../

342/