Main Title

source : Parstoday
Jumapili

17 Septemba 2023

19:29:04
1394178

Rais Steinmeier: Uislamu ni dini ya Ujerumani

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani alisema Jumamosi kwamba Uislamu ni dini ya Ujerumani huku kukiwa na ongezeko la ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu inayochochewa na propaganda za vikundi vya mrengo mkali wa kulia na vyama ambavyo vimetumia vibaya mzozo wa wakimbizi na kujaribu kuzua hofu dhidi ya wahamiaji.

"Uislamu, dini ya Waislamu, maisha ya Waislamu, utamaduni wa Waislamu umekita mizizi katika nchi yetu," Steinmeier alisema katika maadhimisho ya mwaka wa 50 wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Vituo vya Utamaduni wa Kiislamu (VIKZ) huko Cologne." Leo hii Uislamu na Waislamu zaidi ya milioni 5, pia ni sehemu ya nchi yetu," amesema. Steinmeier amedokeza kwamba uhuru wa dini ulimaanisha pia kulinda haki za waumini wote. “Ujerumani ni taifa lisiloegemea upande wowote kiitikadi. Lakini uhuru wa kidini haumaanishi kuwa nchi yetu haina dini. Hapana, inamaanisha kuzipa dini nafasi na kulinda uhuru wa waumini, waumini wote.” Matamshi yake yamekuja kufuatia ripoti ya hivi karibuni iliyosema ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku nchini Ujerumani. Jumla ya matukio 898 ya chuki dhidi ya Uislamu yalirekodiwa nchini Ujerumani mwaka wa 2022, huku idadi ya kesi ambazo hazijaripotiwa ikiwa kubwa, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Juni na shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu mjini Berlin, Alliance Against Islamophobia and Muslim Hostility. Ubaguzi wa rangi ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa Waislamu nchini Ujerumani, huku visa vingi vilivyorekodiwa vikiwahusisha wanawake, kulingana na utafiti huo. Miongoni mwa kesi zilizorekodiwa ni pamoja na mashambulizi 500 ya maneno, ikiwa ni pamoja na kauli za uchochezi, matusi, vitisho na kulazimishwa. Barua kumi na moja za vitisho kwa misikiti na "mara nyingi vitisho vya vurugu na vifo" zilirekodiwa. Barua hizo zilikuwa na alama za Nazi au marejeleo ya enzi ya Nazi. Ripoti hiyo ilibainisha kesi 190 za ubaguzi na 167 za "tabia mbaya." Kundi la mwisho lilijumuisha visa 71 vya kudhuru mwili, visa 44 vya uharibifu wa mali, visa vitatu vya uchomaji moto na vitendo vingine 49 vya ghasia. Kwa kuongezea, mashambulizi yanayochochewa na ubaguzi wa rangi dhidi ya vijana na watoto yanaongezeka. Kuna matukio ambapo wanawake walishambuliwa mbele ya watoto wao na wanawake wajawazito walipigwa au kupigwa kwenye tumbo.

342/