Main Title

source : Parstoday
Jumatano

20 Septemba 2023

18:45:29
1394765

Guterres: Kuna udharura wa kufanyika mageuzi katika Baraza la Usalama la UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho muundo wa taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Antonio Guterres alisema jana Jumanne mwanzoni mwa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York kwamba: Baraza la Usalama lazima lifanyiwe mageuzi kulingana na dunia ya sasa, na muundo wa kifedha wa kimataifa lazima ubuniwe upya.

Guterres alisema kupuuza mageuzi ndani ya taasisi za kimataifa kutachochea mizozo, na kuongeza: Taasisi za fedha za kimataifa zinapaswa kuwa na utandawazi halisi ili ziweze kusaidia kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi zinazoendelea.

Pia ametoa wito wa kuundwa chombo cha kimataifa, sawa na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, kufuatilia maendeleo ya akili bandia (artificial intelligence) duniani na kutoa ripoti kwa nchi zote.

Guterres amesisitiza kuwa: Dunia imejaa changamoto na inaonekana kwamba hatuwezi kukabiliana nazo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametaka hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kutenga rasilimali fedha kwa nchi zinazoendelea kwa matumizi ya nishati safi.

Guterres ameongeza kuwa: Mabadiliko ya hali ya hewa yameweka rekodi mpya na sayari yetu imepata joto kupita kiasi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, na bila ya kulaani uhalifu unaofanywa na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na mienendo ya kibaguzi ya utawala huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, hatua za upande mmoja za Israel ndio sababu ya kudhoofika mchakato wa maridhiano katika kanda ya Mashariki ya Kati.Guterres pia ametoa wito wa kufanyika juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine kwa kutumia njia tofauti. Kuhusu bara la Afrika, Katibu Mkuu wa UN amesema: Mapinduzi yanatishia usalama wa bara hilo. Akizungumzia hali ya Sudan, Antonio Guterres ameonya kuwa: "Nchi hii inaelekea kwenye vita vya upande zote na inakabiliwa na hatari ya kugawanyika. Amesema: "Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, na unyanyasaji wa kijinsia ndio hali ya kutisha ya kila siku katika nchi ambayo imeathiriwa na unyonyaji wa karne nyingi."

342/