Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

23 Septemba 2023

18:28:15
1395376

Hatua mpya ya Russia ya kutumia sarafu za kitaifa na kupunguza utegemezi kwa dola ya Marekani

Serikali ya Russia imeidhinisha orodha ya nchi 31, zikiwemo Iran, Brazil, Venezuela na Cuba, ambazo benki zao zinaweza kushiriki na kufanya biashara katika soko la fedha za kigeni nchini Russia.

Kwa mujibu wa waraka huu wa serikali uliotiwa saini na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin, benki na wawakilishi wa nchi zilizoidhinishwa wanaweza pia kushiriki katika soko la bidhaa zinazotokana na fedha.

Orodha hii inajumuisha Jamhuri ya Azerbaijan, Armenia, Belarus, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan, na Uzbekistan, pamoja na nchi nne za Brazil, India, China na Afrika Kusini, ambazo pamoja na Russia zinaunda kundi la "BRICS". Hali kadhalika nchi zingine zilizojumuishwa na mpango huo wa Russia  ni pamoja Serbia, Uturuki, Iran, Qatar, Pakistan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Morocco na Malaysia. Kulingana na Kremlin, uamuzi huu ulikuwa sehemu ya mfumo wa sheria mpya zilizoidhinishwa Julai iliyopita. ambayo inataka kuongeza ufanisi wa "utaratibu wa ubadilishaji wa moja kwa moja wa sarafu za kitaifa za nchi rafiki na zisizoegemea upande wowote."

Russia imeharakisha juhudi zake za kufanya biashara na nchi nyingine kwa fedha zao kitaifa badala ya sarafu ya dola ya Marekani ili kukabiliana na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo kutokana na vita vya Ukraine.

Kama mwanachama muhimu wa kundi la "BRICS", Russia, pamoja na wanachama wengine wa kundi hilo linalojumuisha nchi  zinazoinukia kiuchumi ambazo ni Brazil, India, China na Afrika Kusini, zinataka kutumia sarafu zao za kitaifa katika shughuli zote za kimataifa za kibiashara. Nchi wanachama wa BRICS zina sababu nyingi za kutumia sarafu zao za kitaifa katika mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara na pia kuunda sarafu mpya.

Changamoto za hivi majuzi za kifedha duniani na sera kali za kigeni za Marekani zimezifanya nchi za BRICS kuchunguza uwezekano huu. Nchi hizo zinataka kuchukua hatua ambazo ni kwa maslahi yao ya kiuchumi huku zikipunguza utegemezi wa kimataifa kwa dola ya Marekani na Euro. Mwishoni mwa Julai 2023, Rais wa Russia Vladimir Putin, alisisitiza umuhimu wa benki ya BRICS katika utaratibu mpya wa kifedha na kusema: "Kuunda taasisi mbadala za kifedha katika wakati ambapo Washington imegeuza dola ya Marekani kuwa silaha ni ngumu lakini ni hatua muhimu."

Putin alisisitiza kuwa nchi za BRICS hazipingani na mtu yeyote, lakini wanachama wake wanafanya kazi pamoja kwa manufaa ya pande zote, ikiwa ni pamoja na katika masuala ya kifedha. Alibainisha kuwa:  Wanachama wa BRICS wanalipana fedha sasa kwa kutumia sarafu zao za kitaifa. Oktoba 2020, Putin pia alisema. Marekani imedharau mfumo wa kimataifa wa fedha kwa kutumia sarafu yake yad ola kama silaha.Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amekiri kuwa vikwazo vinaweza kusukuma baadhi ya nchi kuachana na sarafu ya dola.

Ijapokuwa dola bado ndiyo sarafu kubwa zaidi ya akiba duniani, sera ya  Marekani ya kutumia sarafu yake hiyo kama silaha ya kifedha imeongeza kasi ya nchi nyingi za kuwekeza katika sarafu mbadala.

Nchi nyingi zimekasirishwa na sera ya Marekani ya kutumia sarafu ya dola kushinikiza nchi zenye misimamo huru na zinazopinga ukoloni mambo leo ya madola ya Magharibi. Hivi sasa nchi hizo zimeazimia kutumia sarafu zao za kitaifa ili kukabiliana na uhasama wa Marekani.

Miongoni mwa nchi ambazo zimeazimia kutupilia mbali sarafu ya dola ni China, Russia, India, Brazil, Malaysia, Uturuki, Venezuela na Iran. Nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia pia zimekubali kuitenga dola ya Marekani katika miamala yao yote ya kifedha na kibiashara.

Katika kufanikisha mchakato wa kuitenga zaidi sarafu ya dola, Russia imewasilisha orodha ya nchi 31 ambazo benki zao pamoja na taasisi za kibiashara zinaweza kushiriki na kufanya biashara katika soko la fedha za kigeni kwa sarafu za kitaifa.

Hii ni hatua nyingine ya kutumia sarafu za taifa na kupunguza utegemezi wa dola katika biashara ya kimataifa.

Bila shaka mpango huo wa Russia ni pigo kubwa wa uchumi wa Marekani.



342/