Main Title

source : Parstoday
Jumapili

24 Septemba 2023

14:47:39
1395567

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Uturuki wakutana New York kujadili mgogoro wa Syria

Sambamba na juhudi zinazoendelea za kidiplomasia za kuushughulikia mgogoro wa Syria, mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na Uturuki wamefanya mkutano wa pande tatu katika muktadha wa Mazungumzo ya Astana kwa ajili ya kujadili njia za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mkutano huo wa pamoja umefanyika pembeni ya Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, na Hakan Fidan Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria Geir Pedersen naye pia alihudhuria mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ofisi ya ujumbe wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza katika kikao hicho, Amir-Abdollahian amekosoa vikali kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Syria, akisema sehemu ya masaibu yanayowaandama wananchi wa Syria yanatokana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi na uporaji wa rasilimali na maliasili za nchi hiyo, hatua ambazo zinawaathiri zaidi wanawake na watoto wa taifa hilo, mbali na wananchi wengine.Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikwazo dhidi ya Syria akivielezea kuwa ni "haramu" na kinyume cha sheria na kutilia mkazo haja ya kuondolewa kikamilifu. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameendelea kueleza kwamba ujenzi mpya wa Syria iliyoharibiwa na vita haupaswi kuchukuliwa kama chombo cha kutolea shinikizo kwa serikali ya Damascus, na akaongeza kuwa utatuzi wa mgogoro wa wakimbizi wa Syria unahitaji kurejesha miundombinu muhimu na upatikanaji wa maji, umeme na huduma nyinginezo kwa watu wote. Aidha, amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa inapasa ichukue jukumu lake la kupunguza mateso yanayolitaabisha taifa la Syria. Iran na Russia ambazo ni washirika wa serikali ya Syria, pamoja na Uturuki, ambayo inaunga mkono upande wa upinzani, zilianzisha mchakato wa amani wa Astana mnamo Januari 2017 kwa nia ya kuhitimisha mgogoro wa Syria kupitia ushiriki wa serikali ya nchi hiyo na upinzani.../   

342/