Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Septemba 2023

19:48:01
1396262

Balozi wa Ufaransa nchini Niger arejea makwao baada ya kutimuliwa na utawala wa Niamey

Balozi wa Ufaransa nchini Niger, Sylvain Itté, amewasili katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, leo Jumatano, baada ya utawala wa kijeshi wa Niamey kumtimua nchini humo.

Shirika la Habari la Ufaransa linukuu Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi hiyo ikisema kwamba, Waziri Catherine Colonna amempokea balozi Sylvain Itté katika makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje na kumshukuru kwa kuitumikia nchi yake katika "mazingira magumu.”

Hatua hii imechukuliwa baada ya tangazo la Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Jumapili iliyopita, la uamuzi wa kumrejesha nyumbani balozi wa Paris mjini Niamey "ndani ya masaa kadhaa" na kuondoa vikosi vya Ufaransa kutoka Niger.
Macron pia alitangaza kwamba vikosi vya Ufaransa vitaondoka Niger ifikapo mwisho wa mwaka, akisisitiza kusitishwa ushirikiano wa kijeshi na kile alichokiita mamlaka ya sasa ya Niamey.

Baraza la Kijeshi la Niger limekaribisha tangazo la Ufaransa la nia yake ya kuondoa vikosi vyake nchini humo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, likisema huu ni wakati wa kihistoria na hatua mpya kuelekea uhuru kamili.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Kijeshi la Niger imeeleza kuwa, kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa na balozi wa nchi hiyo nchini Niger ni wakati wa kihistoria na kwamba: "Leo tunaadhimisha enzi mpya katika njia ya uhuru na mamlaka ya kujitawala Niger."Baraza la kijeshi la Niger lilikuwa limeitaka Ufaransa kuondoa wanajeshi wake kutoka Niger ifikapo Septemba 3. Baraza hilo pia lilitishia kwamba vinginevyo baada ya tarehe hiyo, makamanda wa kijeshi wa Ufaransa watawajibika kwa matukio yoyote yatakayotokea. Baada ya kumuondoa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum aliyetambuliwa kuwa kibaraka wa Ufaransa, utawala wa kijeshi nchini Niger ilichukua msururu wa maamuzi dhidi ya Paris ikiwa ni pamoja na kumfukuza balozi wa Ufaransa, kufuta makubaliano ya nchi mbili, na kufunga anga ya nchi hiyo kwa ndege za Ufaransa.