Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Septemba 2023

19:48:33
1396263

Umoja wa Mataifa wakosoa "marufuku ya hijabu" katika Michezo ya Olimpiki 2024

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imekosoa uamuzi wa serikali ya Ufaransa "kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanariadha wa Ufaransa" katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka ujao inayoandaliwa na Paris.

Waislamu walio wachache nchini Ufaransa daima wamekuwa wakikabiliana na mbinyo na vizingiti kuhusiana na masuala yao ya kiibada na kidini, na masharti magumu kwa wanawake wanaovaa vazi la hijabu kwa kuzingatia sheria za kilaiki za Ufaransa.

Katika taarifa yake, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imelaani marufuku ya vazi la hijabu nchini Ufaransa, ikisema kuwa nchi hiyo imekiuka mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu kwa kuwazuia wanawake na wasichana kuvaa hijabu shuleni na maeneo ya umma.

Akizungumzia uamuzi huo wa serikali ya Ufaransa, Marta Hurtado, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, kwa ujumla, kwa mujibu wa sheria ya Kamati ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake, kila nchi mwanachama wa mkataba huu ikiwa ni pamoja na Ufaransa, inalazimika kuchukua hatua zote zinazofaa kurekebisha mifumo yoyote ya kitamaduni na kijamii inayotambua jinsia moja kuwa ni bora au duni kuliko nyingine.

Hurtado amesisitiza kuwa, vitendo vya kibaguzi dhidi ya kundi moja vinaweza kuwa na matokeo mabaya.

Matamshi hayo ya msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa yametolewa baada ya Waziri wa Michezo wa Ufaransa kusema Jumapili iliyopita kwamba, wanariadha wa Ufaransa hawataruhusiwa kuvaa hijabu katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka ujao mjini Paris.

Mwaka 2011, Ufaransa ilipitisha marufuku ya vazi la hijabu, na baada ya hapo, nchi zingine za Ulaya kama Denmark, Austria, Uholanzi na Bulgaria pia zilipitisha sheria kama hizo.

Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ulaya zimezidisha sera za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

342/