Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Septemba 2023

19:50:13
1396264

Wataalamu: Machafuko ya Ethiopia na Sudan yanatishia eneo la Pembe ya Afrika

Mtaalamu wa masuala ya jiografia ya kisiasa ya Afrika Mashariki ameonya kuwa ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika nchi za Ethiopia na Sudan unatishia eneo zima la Pembe ya Afrika na unalielekeza eneo hilo kwenye machafuko zaidi.

Daniel Haley, mtaalamu wa Kimarekani wa masuala ya jiografia ya kisiasa ya Afrika, ameandika makala katika jarida la Marekani la National Interest, akisema kuwa ukosefu wa utulivu na usalama ni mojawapo ya sifa endelevu za hali ya eneo la Pembe ya Afrika.

Haley ameongeza kuwa: Eneo hilo limeshuhudia migogoro mingi, mfano wake ni vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Somalia, vita vya uhuru wa Eritrea, vita vya kujitenga Sudan Kusini, pamoja na migogoro ya hapa na pale kati ya Eritrea na Ethiopia, na machafuko ya sasa ya Sudan na Ethiopia.Mtaalamu huyo wa Marekani ameongeza kuwa: Eritrea ndiyo nchi pekee katika Pembe ya Afrika ambayo bado haijakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na utawala wa mkono wa chuma na wa miongo mitatu wa Rais Isaias Afwerki. Haley amesisitiza kuwa: Eneo hilo halina uwezo wa kustahamili nchi nyingine iliyofeli kama Somalia, na wazo la Sudan au Ethiopia kujiunga na safu ya nchi zilizoshindwa linaweza kuitumbukiza Pembe ya Afrika kwenye dimbwi la kudumu la machafuko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na mapigano ya kijeshi. Amesisitiza kuwa migogoro ya Sudan na Ethiopia inapaswa kupewa mazingatio makubwa na jamii ya kimataifa.