Main Title

source : Parstoday
Jumatano

27 Septemba 2023

19:52:16
1396268

Kumalizika safari ya Amir Abdollahian mjini New York; diplomasia yenye nguvu ndani ya siku 7

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amerejea Tehran baada ya kuwa mjini New York kwa siku saba.

Swali muhimu ni kuwa je, safari ya siku 7 ya Amir Abdollahian mjini New York iliendaje na itakuwa na matokeo gani?

Mikutano ya kidiplomasia na mazungumzo ya kisiasa na vyombo vya habari pamoja na duru za kielimu ilikuwa ajenda muhimu ya safari ya siku 7 ya Amir Abdollahian mjini New York. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa na takriban ratiba 43 mjini New York, ambapo 34 kati ya hizo zilihusu mikutano na mawaziri wenzake na baadhi ya viongozi, ikiwa ni pamoja na kikao na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa yalijadiliwa katika mikutano hiyo. Kikao cha Amir Abdollahian na Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia kilisisitiza azma ya Tehran ya kuboresha na kuimarisha uhusiano wake na Riyadh. Kikao hicho kinaonyesha hamu ya nchi mbili kuendelea na njia iliyoanza Machi iliyopita ya kuhuisha uhusiano wa nchi hizo.

Kikao cha Amir Abdollahian na Jeyhun Bayramov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Azerbaijan, kililenga kutatua matatizo ya pande mbili na masuala ya kieneo, ikiwa ni pamoja na kadhia ya Nagorno Karabakh. Kikao hicho sawa na mikutano na mazungumzo ya awali kati ya pande hizo mbili, kinaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajaribu kudhibiti hitilafu zilizopo kati yake na Azerbaijan kwa njia ya mazungumzo bila kuathiriwa na propganda za vyombo vya habari vya wapinzani na washindani wake wa kieneo.

Kikao cha Amir Abdollahian na Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri mjini New York, pia kilikuwa muhimu sana. Kikao hicho kilichofanyika katika hali ya utulivu, kinaweza kuwa utangulizi wa kufufuliwa uhusiano wa Tehran na Cairo baada ya miongo minne.Kikao cha Amir Abdollahian na Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi pia kinaonyesha azma ya Iran ya kushirikiana na nchi za Kiarabu. Amir Abdollahian ameandika katika ujumbe akiwa mjini New York kuwa siasa za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni za kuimarisha maingiliano na ushirikiano wake chanya na nchi za eneo. Mbali na nafasi ya kijiografia, siasa za ujirani mwema, historia, utamaduni na dini moja, ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo ushirikiano uliosimama juu yake unaweza kudhamini amani, usalama wa kieneo, ustawi wa pamoja kiuchumi na manufaa mengine mengi kwa ajili ya mataifa ya eneo. Kikao kingine muhimu cha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilichofanyika mjini New York, Marekani ni cha kukutana na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje alielezea moja kwa moja na kwa uwazi mkubwa misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na masuala muhimu yanayohusu Iran, eneo na dunia kwa ujumla. Katika uwanja huo, Amir Abdollahian pia aliandika ujumbe kuhusiana na mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusema walijadiliana masuala mengi yakiwemo ya vita vya Ukraine, hali ya Syria, usitishaji vita huko Yemen, ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, mapatano ya JCPOA na juhudi za kuondoa vikwazo, mabadilishano ya karibuni ya wafungwa wa Marekani na Iran, vikwazo haramu na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na umuhimu wa mkutano wa kieneo wa Ghuba ya Uajemi uliopendekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika kikao chake na viongozi wengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya 13 ya Iran amezungumzia baadhi ya changamoto zilizopo duniani na kieneo na kushauriana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tofauti kuhusu kufuatiliwa masuala na makubaliano ya pande mbili ambayo yamefikiwa kati ya Tehran na nchi nyingine. Kwa msingi huo, tunaweza kusema kwamba Amir Abdollahian alitumia vizuri fursa ya safari yake mjini New York kufafanua na kuweka wazi siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, na pia kuwasilisha picha halisi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na wanavyotaka kuonyesha wanafiki na wapinzani sugu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

342/