Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

28 Septemba 2023

16:54:30
1396457

Onyo la Guterres kuhusu ushindani na hatari ya vita vya nyuklia duniani

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu dunia kuingia katika mashindano mapya ya silaha za nyuklia ambayo yanaweza kueneza maafa duniani kote. Katika siku ya mwisho ya mkutano wa mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama amesema mashindano ya silaha yanatia wasiwasi wa kuongezeka karibuni idadi ya silaha za nyuklia ulimwenguni.

Akielezea mashindano mapya ya silaha za nyuklia duniani kama ya kiwendawazimu, Guterres amesema matumizi yoyote ya silaha za nyuklia, wakati wowote, mahali popote na katika mazingira yoyote, yatasababisha maafa ya kibinadamu, na kuwa ni lazima siasa na mwenendo huo ubadilike. Akiashiria kuwepo duniani kwa kipindi kirefu silaha za nyuklia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi zote duniani kuzingatia suala hilo na kutojitumbukiza kwenye janga la maafa ya nyuklia.

Ongezeko la maghala ya silaha za nyuklia duniani, ushindani wa kuzimiliki pamoja na matumizi yake kunapelekea ulimwengu kukabiliwa na hatari kubwa ya silaha hizo. Onyo hilo la nyuklia la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa limetolewa kwa kuzingatia makabiliano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kati ya Russia na Marekani kufuatia vita vya Ukraine, na siasa za Moscow za kuonyesha uwezo wake wa nyuklia zimedhihirisha azma yake ya kukabiliana na vitisho dhidi yake kutoka nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani. Kwa hakika, baada ya vita vya Ukraine, dunia inakabiliwa na jinamizi la vita vya nyuklia kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha Vita Baridi. Russia imekuwa ikionya mara kwa mara juu ya uwezekano wa kutoa maafa ya nyuklia kutokana na siasa za kichochezi za nchi za Magharibi, hasa NATO, kwa uongozi wa Marekani. Katika msimamo wake wa karibuni kuhusu suala hilo, Dmitry Medvedev, Naibu wa Baraza la Usalama la Russia na rais wa zamani wa nchi hiyo, alizungumzia suala la kubadilishwa NATO kuwa kambi kubwa ya  kifashisti hata kuliko kipindi cha Hitler na kuongeza kuwa Russia iko tayari kukabiliana na siasa hizo. Ameonya kwamba matokeo ya vitendo hivyo yatakuwa na madhara makubwa kwa jamii ya mwanadamu kuliko ya mwaka 1945 yaani Vita vya Pili vya Dunia.Mkataba wa Kuzuia Kuenea Silaha za Nyuklia (NPT), ambao ulianza kutekelezwa tokea mwaka 1970, unahesabiwa kuwa ndio wenye wanachama wengi zaidi kati ya mikataba iliyopo ya udhibiti wa silaha duniani, ambapo umetiwa saini na zaidi ya nchi 191. Tangu kuanza kutekelezwa mkataba wa NPT, suala la kutokomeza silaha hizo hatari daima limekuwa kwenye ajenda ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, mkataba huo umekuwa ukipuuzwa sana, hasa na wamiliki wa silaha za nyuklia duniani. Kwa hakika, mojawapo ya changamoto za utekelezaji wa mkataba wa NPT ni kutoheshimiwa vipengee vyake na nchi zenye silaha za nyuklia. Licha ya kuwepo mkataba huo ambao lengo lake ni kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa silaha hizo haribifu, matumizi yake yanaweza kuacha madhara na hasara kubwa kwa jamii ya mwanadamu na mazingira kwa ujumla. Lakini mataifa yenye nguvu za nyuklia yanaendelea kutengeneza silaha hizo za maangamizi makubwa bila kujali hatari hiyo. Hii ni pamoja na kuwa kuongezeka mivutano kati ya mataifa hayo yenye nguvu, hasa kati ya Russia na NATO baada ya vita vya Ukraine, kumezidisha uwezekano wa kutumiwa silaha za nyuklia katika mizozo inayoweza kutokea katika siku za usoni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Moscow ikasisitiza haja ya kuepukwa vita kama hivyo. Awali na katika barua yake kwa washiriki wa mkutano wa NPT, Rais Vladimir Putin wa Russia alionya kuwa hakutakuwa na mshindi katika vita vya nyuklia na kwamba mzozo kama huo haupaswi kuanzishwa.Kwa hakika, dunia imekuwa ikikabiliwa na jinamizi la vita vya silaha za nyuklia kwa zaidi ya miaka 78 sasa na mataifa makubwa ya nyuklia bado yanaendelea kuziimarisha na kuzitengeza upya. Nchi tano zinazotambulika kuwa nchi za nyuklia ambazo ni Marekani, Russia, China, Ufaransa na Uingereza pamoja na nchi zilizojiunga nazo katika miongo ya hivi karibuni zinazalisha, kuimarisha na kuboresha mifumo ya kurusha silaha hizo za maangamizi ya umati. Kuhusiana na jambo hilo huku akizikosoa siasa za madola hayo, Guterres amesisitiza kuwa nchi hizo kwa kuimarisha maghala yao ya silaha, zimefanya kuwa ngumu juhudi za kuzitambua, na kwamba mifumo ya zamani iliyokuwa imeanzishwa kwa ajili ya kuzuia kuenea na kusambaa silaha za nyuklia haifai tena. Tokea utawala wa Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, nchi hiyo ilianza kutekeleza siasa za kukarabati na kuboresha upya silaha zake za nyuklia ambapo siasa na mwenendo huo bado unaendelezwa katika serikali ya Rais Joe Biden wa hivi sasa wa nchi hiyo.