Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

28 Septemba 2023

16:56:10
1396459

Moscow: Tunafuatilia harakati za kijeshi za Marekani huko Baltic

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameitahadharisha Marekani kuhusu kutumwa kwa mifumo ya makombora katika eneo la Baltic na akasema ushirikiano wa Canada na Wanazi utakuwa na athari mbaya katika uhusiano wake na Moscow.

Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Russia amesema kuwa nchi hiyo inafuatilia harakati na shughuli zote za kijeshi za Marekani katika eneo la Baltic. 

Zakharova  amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow kwamba, Russia inafuatilia kwa karibu hatua za Marekani za kujiandaa kutuma mifumo ya makombora mbayo hapo awali ilipigwa marufuku chini ya mkataba Unaopiga Marufuku Makombora ya Nyuklia ya Masafa ya Kati. 

Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, hatua ya Ottawa ya kushirikiana na Wanazi na mashambulizi yake ya kiuhasama dhidi ya Russia haitasalia hivi hivi bila ya majibu. Amesema  kitendo hicho cha Ottawa kitaathiri uhusiano kati ya Russia na Canada.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa uhusiano wa Moscow na Ottawa unakabiliwa na mgogoro mkubwa kutokana na msimamo wa viongozi wa nchi hiyo. "Tunaiona Canada kama nchi isiyo na rafiki kabisa ambayo viongozi wake wamejitia doa kwa kushirikiana na Unazi na kusaliti historia yao", amesema Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia." Bunge  la Canada Ijumaa iliyopita lilimpa hadhi na kumkaribisha bungeni Mnazi raia wa Ukraine ambapo alishangiliwa  na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na  Rais wa UKraine, Volodymyr Zelensky.