Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

29 Septemba 2023

22:17:56
1396692

Umoja wa Mataifa wakosoa hatua mpya ya Ufaransa dhidi ya hijabu ya Kiislamu

Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Jumatano alikosoa marufuku ya uvaaji hijabu kwa wanariadha wa Ufaransa katika michezo ya Olimpiki ya 2024, ambayo imepangwa kufanyika Paris mwaka ujao.

Hurtado amesema: "Hakuna mtu aliye na haki ya kuwalazimisha wanawake wavae anavyotaka yeye. Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, marufuku ya kujieleza na kutoa maoni ya kidini, kama ilivyo marufuku ya mavazi, inaweza kutekelezwa tu pale inapotishia usalama wa umma au afya ya jamii, na hii ni katika hali ambayo vazi hilo la stara kwa wanawake wa Kiislamu halikiuki jambo hilo."

Ukosoaji huo unafuatia hatua ya waziri wa michezo wa Ufaransa aliyetangaza kuwa wanariadha wa nchi hiyo watapigwa marufuku kuvaa hijabu wakati wa michezo ya Olimpiki ya Paris mwakani ili kuendana na sheria za nchi hiyo za kutofuata misingi ya dini. Uamuzi huo umekabiliwa na wimbi la ukosoaji wa wanariadha wa Kiislamu wa Ufaransa. Paris tayari imepiga marufuku uvaaji wa abaya kwa wasichana katika shule za wasichana kuanzia Septemba 2023.Laicite ni aina ya ulaiki unaopindukia mipaka na serikali ya Ufaransa, kwa mujibu wa sheria ya Laicite iliyopasishwa 1905, ambayo inasema kwamba dini haiingilii mambo ya serikali na serikali masuala ya kidini, inajaribu kuzifuta taasisi zote za kidini katika maeneo ya umma na idara za serikali. Kupiga marufuku uvaaji wa hijabu katika shule na vyuo vikuu pamoja na hafla za michezo ni mfano wa fikra hizo zenye utata. Nchini Ufaransa, ni marufuku kuhudhuria shule na taasisi za serikali ukiwa na nembo za kidini, na kuvaa hijabu kumepigwa marufuku katika shule za umma tangu 2004 chini ya sheria hiyo. Katika hali ambayo vyama vya mrengo wa kulia vya Ufaransa vinasisitiza kupiga marufuku hijabu ya Kiislamu, wanasiasa wa mrengo wa kushoto wana wasiwasi kuhusu haki za wanawake na wasichana wa Kiislamu.

Ukosoaji wa Umoja wa Mataifa dhidi ya wanariadha wa Ufaransa kunyimwa haki ya kuvaa hijabu kwa hakika ni muhuri wa kubatilisha madai ya serikali ya Ufaransa, kuwa inaheshimu misingi ya uhuru na haki sawa kwa raia wote wa nchi hiyo. Ni muda mrefu sasa ambapo, wanawake na wasichana wa jamii ya Kiislamu nchini Ufaransa ambayo inaunda idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya, wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi, mashinikizo na vikwazo vya kila aina kutokana na kuvaa kwao hijabu, vikiwemo vya kupigwa marufuku kusoma wakiwa wamevaa hijabu. Hatua ya hivi karibuni ni ile ya kupigwa marufuku wasichana wa Kiislamu kuvaa abaya katika shule za Ufaransa. Gabriel Attal, Waziri wa Elimu wa Ufaransa, alipokuwa akitangaza kupiga marufuku uvaaji wa abaya kwa wasichana katika shule za nchi hiyo, alidai kuwa abaya inakiuka sheria za kisekula za Ufaransa kuhusiana na suala la elimu.

Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na kushadidi mashinikizo dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa umeongezeka pakubwa katika miaka ya hivi karibuni. Katika uongozi huu wa Emmanuel Macron, rais wa mrengo wa kati wa Ufaransa, vikwazo hivyo vimeongezeka sambamba na kupitishwa sheria nyingi dhidi ya Waislamu na vituo vya Kiislamu na hivyo kufanya maisha ya Waislamu nchini humo kuwa magumu sana. Mnamo Februari 2022, serikali ya Ufaransa ilitangaza kuunda shirika jipya linaloitwa "Baraza la Kiislamu la Ufaransa" kwa madai ya kuwafungamanisha Waislamu wa nchi hiyo na utamaduni na jamii ya Ufaransa pamoja na kupambana na misimamo mikali.Kuanzishwa baraza hilo ni sehemu ya juhudi kubwa za Rais Emmanuel Macron za kuudhoofisha Uislamu nchini Ufaransa. Taasisi iliyotangulia iliyokuwa ikifanya kazi chini ya anwani ya "Baraza la Madhehebu ya Kiislamu ya Ufaransa" ilivunjwa. Mtazamo na hatua hizo za Macron zinatekelezwa kwa msingi wa "usekula wa kuhujumu" ambapo unataka kukabiliana moja kwa moja na dini na nembo za kidini katika jamii. Kimsingi, serikali ya Ufaransa haina mtazamo mzuri kuhusu Uislamu, hivyo imekuwa ikiunga mkono hatua yoyote inayochochea chuki dhidi ya Uislamu, ikiwemo ya karibuni ya kupiga marufuku vazi la hijabu ya Kiislamu shuleni na sasa katika michezo ya Olimpiki.