Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

30 Septemba 2023

19:09:59
1396885

UN yatuma ujumbe wake Nagorno-Karabagh kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 30

Umoja wa Mataifa utatuma ujumbe katika eneo la Nagorno-Karabakh kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 30, kufuatia makubaliano uliyofikia na Serikali ya Azerbaijan juu ya suala hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujjaric amewaeleza waandishi wa habari kuwa, ujumbe huo utaelekea eneo la Karabakh mwishoni mwa wiki hii kujionea hali halisi wakati huu ambapo watu wanakimbia kwa hofu ya usalama wao kwenye eneo hilo linalozozaniwa kati ya Azerbaijan na Armenia, nchi ambazo zamani zilikuwa chini ya Muungano wa Kisovieti.

Dujarric amesema ujumbe huo utaongozwa na Mratibu Mkazi wa UN nchini Azerbaijan, Vladanka Andreeva, na Mkurugenzi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu, OCHA  Ramesh Rajasingham pamoja na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Armenia, ikiongozwa na Kaimu Mratibu Mkazi Nanna Skau, inashirikiana na serikali ya nchi hiyo kusaidia wimbi la wakimbizi wanaovuka mpaka na kuingia nchini humo kutoka eneo la Karabakh. Takwimu za hivi punde zaidi zinasema takribani watu 93,000 wamevuka mpaka na kuingia Armenia.Tangazo la UN la kutuma ujumbe wake huko Nagorno-Karabagh limekuja baada ya ombi la Armenia kwa Mahakama ya Dunia kuitaka iiamuru Azerbaijan iondoe wanajeshi wake wote katika vituo vya kiraia kwenye eneo hilo ili Umoja wa Mataifa upate njia yenye usalama kwa ajili ya kuwafikia raia. Hayo yalielezwa na mahakama hiyo hapo jana.

Mahakama ya Dunia, inayojulikana rasmi kama Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), mnamo mwezi Februari iliiamuru Azerbaijan ihakikishe kwamba watu wanatembea kwa uhuru kupitia ukanda wa Lachin kwenda na kutoka eneo lenye mgogoro, katika hatua ambayo wakati huo ilikuwa ni ya muda kwa ajili ya kutatua mabishano ya kisheria yaliyopo baina na nchi hiyo na jirani yake Armenia.

Wiki iliyopita, vikosi vya Azerbaijan vilichukua udhibiti wa eneo hilo lililojitangazia mamlaka, ambalo wakazi wengi wana asili ya Armenia, na kusababisha wakazi hao kukimbia na kuzusha hofu ya kuzuka uangamizaji wa kimbari.../


342/