Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

30 Septemba 2023

19:12:51
1396892

Tokea kuanza Intifadha ya Al-Aqsa hadi leo; kuimarika muqawama wa Palestina na kudhoofika Israeli

Miaka 23 imepita tokea kuanza Intifadha ya Al-Aqsa. Swali muhimu ni kwamba, je, miaka 23 baada ya Intifadha ya Al-Aqsa, ni matukio gani yameshuhudiwa katika mgogoro wa Palestina na Wazayuni.

Mnamo Septemba 28, mwaka 2000, Ariel Sharon, ambaye alikuwa mkuu wa mrengo wa upinzani wa Utawala wa Kizayuni wakati huo, akiungwa mkono na vikosi maalumu vya usalama 2,000 na polisi wa Kizayuni, aliushambulia na kuuvunjia  heshima Msikiti wa Al-Aqsa kwa uungaji mkono wa Ehud Barak, waziri mkuu wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni. Baada ya shambulio hilo, Sharon alisema kwamba sehemu hiyo ingekuwa mali ya Israeli milele.

Matamshi hayo ya kichochezi yaliwasha moto wa hasira ya Wapalestina, na baada ya hapo kukatokea mapigano makali, ambapo Wapalestina 7 waliuawa shahidi na wengine 250 kujeruhiwa. Katika upande pili pia, askari 13 wa Kizayuni walijeruhiwa.  Baada ya hapo, mji wa Baitul Muqadas ukawa uwanja wa mapigano makali baina ya Wapalestina na walowezi wa kizayuni, ambapo makumi ya watu walijeruhiwa, na harakati ya mapambano iliyokuja kujulikana baadaye kama Intifadha ya Al Aqsa ilianza na kuzidi kupanuka na kuenea hadi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Intifadha ya Al-Aqsa ilidumu kwa kipindi cha miaka 5 hadi kufikia 2005. Kwa mujibu wa takwimu za taasisi za Palestina na Kizayuni, Wapalestina 4,412 wameuawa shahidi na wengine 48,322 kujeruhiwa katika Intifadha ya Al-Aqsa, na vilevile Wazayuni 1,100 wameuawa, wakiwemo wanajeshi 300, na wengine karibu 4,500 walijeruhiwa.Tangu intifadha ya al-Aqsa hadi sasa, utawala ghasibu wa Kizayuni umetekeleza mashambulizi mengi  dhidi ya Wapalestina. Hadi mwaka jana, mashambulizi yote yalikuwa yakielekezwa  Ukanda wa Gaza. Lakini tangu wakati huo, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan pia umekuwa ukilengwa na utawala uvamizi wa Quds. Sababu kuu ya jambo hilo ni kuanza harakati za muqwama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika miaka ya hivi karibuni na kuanzishwa kwa makundi  mbalimbali katika eneo hilo ambapo  mashambulizi mengi huko Tel Aviv yamekuwa yakitekelezwa na makundi hayo ya kimuqawama katika eneo hilo. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa kuingia silaha katika Ukingo wa Magharibi na kuanzishwa makundi ya mapambano katika eneo hilo ni nukta muhimu zaidi katika mzozo wa Palestina na Israeli katika kipindi cha miaka 23 iliyopita. Kuhusiana na hilo, Tareq Salmi, Msemaji wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, aliashiria Alkhamisi katika mahojiano na shirika la habari la Iranpress huko Gaza,  msimamo wa muqawama baada ya miaka ishirini na mitatu ya Intifadha ya Al-Aqsa na kuongeza kuwa nguvu na irada ya makundi ya muqwama  katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, hasa huko Quds tukufu, imeiongezeka pakubwa. Salmi ameongeza kuwa, Brigedi ya Quds, tawi la kijeshi la harakati hiyo, imevunja njama na operesheni za  Wazayuni katika  Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Msikiti wa Al-Aqsa baada ya miaka mingi, na kwamba kundi hilo limejipanga kikamilifu kukabiliana na jinai za walowezi wa Quds Tukufu.

Jambo jengine muhimu ni kwamba silaha muhimu zaidi za Wapalestina katika Intifadha ya Al-Aqswa zimekuwa ni mawe na visu, lakini leo hii makundi ya Wapalestina yanatumia makombora mabalimbali katika mashambulizi yao dhidi ya taasisi muhimu huko Tel Aviv, ambapo walowezi wa Kizayuni wanalazimika kukimbilia maeneo ya maficho katika kila shambulizi. Kwa hivyo, uwezo wa hivi sasa wa makundi ya muqawama ya Palestina hauwezi kulinganishwa na kipindi cha Intifadha ya Al-Aqsa, ambapo hata  kijiografia mashambulizi ya Wapalestina yanafika hadi Tel Aviv.

Jambo jengine ni kuwa, taratibu  hali ya ndani hivi sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu imekuwa tete kwa kadiri kwamba viongozi wa utawala huo wanatahadharisha kuhusu hatari ya kusambaratika utawala huo. Mshikamano ndani ya utawala wa Kizayuni umepotea na hitilafu za ndani kuongezeka sana kwa kadiri kuwa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita utawala huo umefanya chaguzi 5 na kuchaguliwa mabaraza kadhaa ya muda ambapo baraza la sasa la mawaziri  linaloongozwa na Netanyahu pia, liko katika hali ya kuyumbayumba.