Main Title

source : Parstoday
Jumapili

1 Oktoba 2023

21:30:27
1397224

Mlipuko wa bomu watokea karibu na Bunge la Uturuki mjini Ankara

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki imesema magaidi wawili wameshambulia kwa bomu mbele ya majengo ya wizara hiyo iliyo karibu na Bunge katika mji mkuu, Ankara.

Saa chache kabla ya  Bunge la Uturuki kuanza tena vikao vyake baada ya miezi mitatu ya mapumziko, mshambuliaji wa kujitoa mhanga amejilipua karibu na eneo lenye majengo ya bunge na ofisi nyingi za serikali kwenye mji mkuu Ankara.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema shambulio hilo limewahusisha watu wawili mbele ya majengo ya wizara ya mambo ya ndani jijini Ankara, na ameongeza kusema kuwa, mmoja wa washambuliaji hao  alikufa kwenye mlipuko huo na mwingine alidhibitiwa na maafisa wa usalama.

Maafisa wawili wa polisi wamejeruhiwa kidogo kwenye shambulio hilo. Maafisa hao wawili wa polisi wanatibiwa hospitalini na hawako katika hali mbaya, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya hakutoa taarifa za mara moja iwapo mashambulio hayo yanawahusisha wapiganaji wa Kikurdi au makundi ya wapiganaji wanaoegemea mrengo mkali wa kushoto au kundi la kigaidi la Daesh ambalo limehusika na mashambulio mabaya kote nchini Uturuki hapo awali. Waziri Yerlikaya amesema washambuliaji walifika katika eneo la tukio wakiwa ndani ya gari dogo la biashara. Picha za televisheni zilionyesha vikosi vya kutegua mabomu vikifanya kazi karibu na mahala ambako gari hilo liliegeshwa katika eneo ambalo liko karibu na Bunge Kuu la Uturuki na majengo mengine ya serikali. Mwaka mmoja uliopita mshambuliaji wa kujitoa mhanga alijilipua kwenye mji wa Istanbul ambapo kwa akkali watu sita waliuawa na wengine 81 walijeruhiwa. Mshambuliaji huyo alijilipua kwenye eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa huo wa Istanbul mnamo Novemba 13, 2022. Bunge la Uturuki lilipangwa kufunguliwa tena baada ya mapumziko ya miezi mitatu katika msimu wa kiangazi hii leo Jumapili 01/10/2023 na rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan.

342/