Main Title

source : Parstoday
Jumapili

1 Oktoba 2023

21:32:09
1397225

Umuhimu wa kupasishwa rasmi jina la Palestina katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, (IAEA) katika kikao chake cha 67 cha kila mwaka huko Vienna, umepiga kura ya kuunga mkono azimio la kupasishwa rasmi jina la "Nchi ya Palestina"

Wakala huo pia umekubali kutambua haki ya Palestina na kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi hiyo pamoja na nchi zingine za ulimwengu. Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa rasimu iliyopendekezwa na Misri. Misri ilikuwa imetaka kutpasishwa rasmi jina la "Nchi ya Palestina" katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Nchi 92 zimepiga kura kuunga mkono rasimu azimio hilo chini ya kichwa "Hadhi ya Palestina" katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Hii ni katika hali ambayo  nchi  21 zimejizuia kupiga kura hilo na tano tu zimelipinga.

Baada ya kupitishwa azimio hilo kwa kura za 'ndiyo', Mohammad Al-Molla, balozi wa Misri nchini Austria na ambaye pia ni mwakilishi wa Cairo katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, alisema kwamba upasishaji huo umefanyika kwa uungaji mkono kamili wa Kundi la 77 na China. Al-Molla amekuelezea kupitishwa rasmi jina la nchi ya Palestina katika wakala wa IAEA kuwa ni "Azimio la Kihistoria" na kusema kuwa hatua hii inaoneysha ushindi iliopata kadhia ya Palestina. Mohammad Al-Molla ameongeza kuwa hatua hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa Palestina na Wakala wa IAEA na nchi zingine katika uwanja wa teknolojia na sayansi ya nyuklia.

Hatua hiyo imechukuliwa kwa muktadha wa juhudi zinazofanywa na viongozi wa Palestina za kupata uanachama kamili katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na mashirika mengine ya kimataifa. Weledi wa mambo wameutathmini uamuzi huo wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa ni sawa na kuuzaba kibao cha uso utawala wa Kizayuni na ushindi kwa taifa la Palestina.

342/