Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

2 Oktoba 2023

19:16:21
1397476

Uturuki bado inatafuta fursa kwa kuendelea kukalia ardhi ya Syria

Ankara imetangaza kwa mara nyingine kuwa serikali ya Uturuki itaanzisha tena mazungumzo yake na Iran na Russia kwa lengo la kuboresha uhusiano na Syria.

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yashar Güler amesema Ankara iko tayari kuanzisha tena mazungumzo kati ya mawaziri wa ulinzi wa Uturuki, Russia, Iran na Syria. Waziri huyo ameongeza pia kuwa, serikali ya Rais Erdoğan daima iko tayari kuzungumza na kuketi kwenye meza ya mazungumzo kuhusu suala hilo. Lakini ni wazi kuwa masuala ya Syria si jambo linaloweza kutatuliwa mara moja.

Hii si mara ya kwanza kwa afisa wa serikali ya Ankara kuzitaka Iran na Russia kushiriki katika mazungumzo kuhusu uhusiano wa Uturuki na Syria, na maafisa wa baraza la mawaziri la serikali ya Ankara wamekuwa wakitoa matamshi ya mara kwa mara kuhusu uhusiano wa Uturuki na Syria. Huko nyuma, mazungumzo chanya yamefanyika kuhusu utatuzi wa mzozo wa Uturuki na Syria na hatua za pande zote mbili kuchukuliwa kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Ankara na Damascus.

Wataalamu wa duru huru za kisiasa wanalichukulia ombi la serikali ya Uturuki la kutaka kufanya mazungumzo na Iran pamoja na Russia kuhusiana na Syria kuwa ni juhudi  nyingine za viongozi wa serikali ya Ankara za kupata upendeleo kutoka kwa nchi hizi mbili zinazodhamini usalama wa maeneo muhimu ya Asia Magharibi. Ni dhahiri kwamba kujitafutia fursa huko kuna maana ya kufunika suala la kukaliwa ardhi ya Syria na jeshi la Uturuki. Lakini ukweli ni kwamba Uturuki haina budi ila kukomesha ukaliaji huo wa mabavu wa ardhi ya Syria. Hii ni kwa sababu kuwepo kijeshi Syria, kunaigharimu Uturuki mamia ya mamilioni ya dola kwa mwaka, na katika mgogoro wa sasa wa kiuchumi, serikali ya Erdogan haiwezi kumudu gharama hizo. Bila shaka, katika muktadha huu, misaada ya serikali za Kiarabu kwa Uturuki kwa ajili ya kuendeleza kukaliwa Syria kwa mabavu haipaswi kupuuzwa.Hata hivyo, inaonekana kwamba viongozi wa serikali ya Ankara wanajaribu kujipatia fursa ya aina yoyote kutoka kwa Iran na Russia ili inapolazimika ijiondoe salama huko Syria. Katika uwanja huo, Talib Ibrahim, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa wa Syria alisema katika mahojiano yake ya hivi karibuni na Sputnik Arab kwamba Iran na Russia zinaweza kutoa dhamana kwa Uturuki kuhusiana na suala la Wakurdi nchini Syria.

Licha ya siasa zinazogongana za serikali ya Uturuki kuhusiana na suala la kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki pamoja na kutoa pendekezo la kufanya mazungumzo na Iran na Rassia, amesisitiza juu ya kuendelea kuwepo kijeshi nchi yake kaskazini mwa Syria.Hii ina maana kwamba Uturuki haiko tayari kuondoka Syria, na kuwa nchi zinazodhamini usalama wa maeneo muhimu ya Asia Magharibi, zinapaswa kukubali masharti yake na kuipatia dhamana serikali ya Erdogan kuhusiana na jambo hilo. Serikali ya Recep Tayyip Erdogan ilikalia maeneo ya kaskazini mwa Syria na Iraq kwa kisingizio cha kukabiliana na Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan cha Uturuki (PKK). Huku ikipinga hatua za kijeshi za Uturuki, serikali ya Damascus imeeleza mara kwa mara kuwa uwepo wa wanajeshi wa Uturuki kaskazini mwa Syria unakiuka mamlaka ya ardhi ya nchi hiyo na kwamba sharti la kuboreshwa uhusiano wa Ankara na Damascus ni kuondoka wanajeshi wa Uturuki nchini humo. Hatupaswi kupuuza uwezekano kwamba serikali ya Erdogan, kwa kuomba mazungumzo na Iran na Russia kuhusu jambo hilo, inajaribu kuibua masuala ya pembeni ili kufikia malengo yake ya muda mrefu. Pamoja na hayo serikali za Tehran na Moscow zinaonekana kuwa macho zaidi kuhusiana na malengo halisi ya serikali ya Ankara katika uwanja huo.

342/