Main Title

source : Parstoday
Jumatano

4 Oktoba 2023

17:36:04
1397918

WHO yaunga mkono chanjo mpya ya malaria

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amependekeza upanuzi wa utoaji wa chanjo ya malaria duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom, sambamba na kupendekeza matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria iliyopewa jina la  RTS,S, amesema WHO pia inapendekeza chanjo ya pili iitwayo R21/Matrix-M ili kuzuia malaria kwa watoto walio katika hatari ya ugonjwa huu.

Adhanom ameongeza kuwa: Ushahidi unaonyesha kuwa, katika maeneo ambayo maambukizi ni ya msimu, malaria hupungua kwa 75% baada ya dozi 3 za chanjo ndani ya miezi 12. Majaribio yameonyesha kuwa kudunga dozi ya nne mwaka mmoja baada ya dozi ya tatu hudumisha kinga. Amesisitiza kuwa, majaribio haya yameonyesha kuwa chanjo hii ni ya kuaminika na ufuatiliaji wake wa usalama unaendelea wakati wa usambazaji.

Akitangaza kuwa takribani nusu ya dunia bado iko katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa malaria, Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ameeleza kuwa: "Tangu mwaka 2000 vifo vinavyotokana na malaria vimepungua kwa zaidi ya nusu, na tumefanikiwa kutokomeza malaria katika maeneo mengi ya dunia."

Kwa uchache nchi 28 za bara la Afrika zinapanga kutoa chanjo ya malaria iliyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani kama sehemu ya mipango yao ya kitaifa ya chanjo.

Chanjo ya  RTS,S itasambazwa katika baadhi ya nchi za Afrika kuanzia mapema mwaka ujao, na chanjo ya R21 yumkini ikapelekwa katika nchi mbalimbali katikati ya mwaka ujao.

342/