Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

6 Oktoba 2023

15:48:11
1398391

UN na ICRC: Lazima kuweko na sheria na vikwazo kudhibiti silaha zinazojiendesha

Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani ICRC zimetoa wito wa kuanzishwa sheria na vikwazo ili kudhibiti mifumo ya silaha zinazojiendesha.

Katika taarifa yao ya pamoja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Kamati ya ICRC, Mirjana Spoljaric, wamewataka viongozi wa kisiasa kuanzisha haraka sheria mpya za kimataifa kuhusu mifumo ya silaha zinazojiendesha, ili kulinda ubinadamu.

Guterres na Spolijaric wamesema: "leo tunaunganisha sauti zetu kushughulikia kipaumbele cha dharura cha kibinadamu. Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, tunatoa wito kwa mataifa kudhibiti na kuweka vikwazo maalumu kwa mifumo ya silaha zinazojiendesha, ili kukinga vizazi vya sasa na vijavyo kutokana na matokeo ya matumizi yao. Katika mazingira ya sasa ya usalama, kuweka bayana mistari myekundu ya kimataifa kutanufaisha mataifa yote.”Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya UN na ICRC, mifumo ya silaha inayojiendesha ni ile ambayo inaeleweka kwa ujumla kama mifumo ya silaha inayochagua shabaha na kutumia nguvu bila uingiliaji wa binadamu, na inaleta wasiwasi mkubwa wa kibinadamu, kisheria, kimaadili na usalama. Taarifa ya taasisi hizo mbili muhimu kimataifa imetahadharisha kuwa, kuundwa na kuenea kwa silaha hizo kuna uwezekano wa kubadilisha kwa kiasi kikubwa jinsi vita vinavyopiganwa na kuchangia kukosekana kwa utulivu wa kimataifa na kuongezeka kwa mivutano ya kimataifa. Guterres na Spolijaric wamesisitiza kwa kusema: "wasiwasi wetu umetiwa nguvu na kuongezeka kwa upatikanaji na ufikiaji wa teknolojia za kisasa na zinazoibuka kama vile roboti na teknolojia za akili mnemba, ambazo zinaweza kuunganishwa katika silaha zinazojiendesha.” Wawili hao wamehitimisha taarifa yao hiyo kwa kusema: "tunatoa wito kwa viongozi wa dunia waanzishe mazungumzo ya chombo kipya kinachofunga kisheria ili kuweka marufuku na vizuizi vilivyo bayana kwa mifumo ya silaha zinazojiendesha na kuhitimisha mazungumzo kama haya ifikapo 2026. Tunahimiza nchi wanachama kuchukua hatua madhubuti sasa ili kulinda ubinadamu wote".../

342/