Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

26 Oktoba 2023

16:06:33
1405372

Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Marekani ni mshirika katika uhalifu wa Israel

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia dhulma inayokabiliwa na subira na ukakamavu wa wananchi wa Gaza dhidi ya jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Safari za mara kwa mara za marais wa Marekani na nchi nyingine za shari na dhalimu kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni jaribio la kuzuia kusambaratika utawala huo ghasibu.

Ayatullah Ali Khamenei, aliyasema hayo jana Jumatano katika kikao na washiriki wa kongamano la kumbukumbu ya mashahidi 6,555 wa mkoa wa Lorestan, magharibi mwa Iran. Ayatullah Ali Khamenei ameitaja Marekani kuwa ni mshirika halisi katika uhalifu unaofanywa na watendajinai wa Kizayuni na amesisitiza kuwa: "Mikono ya Wamarekani imejaa damu za watoto, wanawake na mashahidi wengine wa Gaza hadi kwenye vifundo vya mkono, na kwa hakika Wamarekani ndio wanaosimamia uhalifu huo."Matamshi hayo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yanaashiria hali halisi ya matukio ya hivi sasa ya Palestina ambayo kwa mara nyingine tena yanafichua nafasi ya nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani katika kuunga mkono kikamilifu jinai na uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel na jitihada zao za kuunusuru usisambaratike.

Hivi sasa, katika kukabiliana na fedheha ya kushindwa kijeshi, kiusalama na kijasusi na wapigania ukombozi wa Palestina katika operesheni ya Kimbunga ya Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni wa Israel unalenga miundombinu muhimu na makazi ya raia wa Ukanda wa Ghaza kwa mashambulizi ya kinyama kwa kutumia mabomu na makombora ya kisasa; matokeo yake, zaidi ya Wapalestina 6,000 wameuawa shahidi na zaidi ya 20,000 wamejeruhiwa. Hii ni pamoja na ukweli kwamba, mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza yasingeweza kuendelea kwa ukatili mkubwa unaoshuhudiwa sasa bila ya himaya na uungaji mkono wa Marekani na nchi za Ulaya, na udhaifu wa mashirika ya kimataifa. Safari mfululizo za viongozi wa Marekani akiwemo rais, waziri wa mambo ya nje na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo mjini Tel Aviv na kushiriki kwao katika mikutano ya baraza la vita la utawala wa Israel ambako hakujawahi kutokea katika kipindi cha miaka 75 iliyopita, vinaonyesha waziwazi ushiriki mkubwa wa Marekani katika vita vya Gaza.

Gazeti la lugha ya Kiebrania la Yedioth Ahronoth limechapisha ripoti kuhusu suala hili na kuandika kwamba: "Washington inaongoza vita vya sasa vya Gaza, badala ya Tel Aviv, kulingana na maslahi yake katika eneo hilo."

Marekani, bila shaka yoyote, ndiyo muungaji mkono mkubwa zaidi wa kisiasa na mdhamini wa silaha wa utawala wa Kizayuni tangu mwanzo mwa kuundwa utawala huo bandia, na silaha zinazotengenezwa na nchi hiyo zina nafasi muhimu sana katika kukidhi mahitaji ya zana za kkivita za Israel. Katika siku za hivi karibuni pia, Marekani imetuma meli mbili za kubeba ndege za kivita za "Gerald Ford" na "USS Eisenhower" katika Bahari ya Mediterania, na vifaa vyake vyote vikiwemo vifaa vya satalaiti, zana za ujasusi na kunasa sauti vimewekwa kwenye huduma ya timu ya vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel.Wakati huo huo, nchi za Ulaya na Marekani zinatumia ushawishi wao katika vikao vya kimataifa ili kuzuia kusimamishwa mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Katika mkondo huo, Marekani pamoja na Uingereza na Ufaransa zimepinga rasimu iliyopendekezwa na Russia kwa ajili ya kuulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel usimamishe mashambulizi dhidi ya watu wa Gaza.

Kwa msingi huo, kwa kuzingatia idadi kubwa ya wahanga wa kiraia wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, hapana shaka yoyote kwamba Marekani inabeba dhima ya kimataifa katika suala hilo. Ibara za 8, 16, 17 na 18 za Hati ya Tume ya Kimataifa ya Sheria iliyoidhinishwa mwaka wa 2001, zinaibebesha dhima nchi au mashirika yasiyo ya kiserikali yanayosaidia kwa namna fulani katika kutenda uhalifu wa kimataifa.