Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

2 Novemba 2023

15:47:53
1407840

Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: "Mauti kwa Marekani" si nara tu bali ni msimamo imara

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika mkutano na maelfu ya wanafunzi waliotoka katika pembe zote za Iran, ameyataja matukio ya tarehe 13 Aban 1358 (November 4, 1979) kuwa pigo la Taifa la Iran kwa Marekani.

Katika kukaribia kumbukumbu ya siku hiyo ambayo inajulikana nchini Iran kuwa Siku ya Wanafunzi na Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Uistikabari,  siku ya Jumatano wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi walikutana na Ayatullah Sayyid  Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Tarehe 13 Aban ni kumbukumbu ya matukio matatu muhimu katika historia ya Iran; kuhamishwa Imam Khomeini (RA) kutoka Iran hadi nchini Uturuki mnamo  4 November 1964, kuuawa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Tehran mnamo Novemba 4 1978, na kutekwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran mnamo Novemba 4, 1979, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiisalmu. Matukio hayo matatu yalikuwa na nafasi maalumu katika kuchagiza harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Utambulisho wa matukio yote matatu ni mapambano dhidi ya madola ya kibeberu na kiistikbari pamoja na vibaraka wao, na kwa msingi huo, siku hii pia inaitwa Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Uistikbari.

Ayatullah Khamenei katika sehemu ya matamshi yake wakati wa mkutano huo wa jana alichambua chanzo cha uadui wa Marekani kwa taifa la Iran na kusema: “Licha ya Wamarekani na wale ambao kwa ujinga au kwa nia nyingine wanakariri kuwa chanzo cha uadui na njama za Marekani ni kutekwa ubalozi wa nchi hiyo, lakini madai haya ni ya uongo kabisa, kwa sababu ukweli wa kihistoria unaonyesha kuwa uadui wa Wamarekani kwa taifa la Iran ulianza miaka 26 kabla ya kutekwa ubalozi huo, yaani tokea mapinduzi ya kidhalimu ya tarehe 15 1953 dhidi ya serikali ya kitaifa ya Dakta Mossadegh.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria nyaraka zilizopatikana katika ubalozi wa Marekani mjini Tehran na kusema: "Nyaraka hizi zinaonyesha kuwa ubalozi wa Marekani, tangu siku za mwanzo za ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, yaani miezi kumi kabla ya kutekwa ubalozi huo, ulikuwa kitovu cha njama na ujasusi, kupanga kuyaangusha mapinduzi ya Kiislamu, kuibua vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusimamia vyombo vya habari vilivyopinga Mapinduzi. Kwa hiyo, uadui wa Marekani na taifa la Iran una sababu nyingine."

Historia ya sasa ya Iran ina ushahidi wa wazi ya njama, vitendo vya uhasama na uingiliaji wa Marekani. Mapinduzi ya Agosti 15 1953, kuunga mkono na kuimarisha misingi ya utawala wa kiimla wa Shah, kuunda shirika la kikatili na kijasusi la ufalme wa Shah maarufu kama SAVAK na kuilazimisha Iran kuwa na sheria za kikoloni na za usaliti ni miongoni mwa hatua za Marekani dhidi ya Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979. Hatua hizo zilichukuliwa na Marekani  kwa lengo la kuitawala na kuwa na satwa juu ya Iran kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

Katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ubalozi wa Marekani ulikuwa kituo cha ujasusi na kupanga njama hadi ulipotekwa na wanafunzi. Nyaraka zilizopatikana katika ubalozi huo ambao wanamapinduzi waliupa lakabu ya 'Pango la Ujasusi' pia zinaonyesha kuwa, ubalozi wa Marekani ulipinga ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kwa hakika ulikuwa kitovu cha njama za kuyashambulia Mapinduzi ya Kiislamu na kudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baada ya kushindwa kusambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani iliuchochea utawala wa Baath wa Iraq kuishambulia Iran. Watawala wa Marekani waliunga mkono utawala huo wa Saddam  na kusababisha vita vya miaka 8 dhidi ya Iran. Hali kadhalika wakati wa vita hivyo, meli ya Marekani iliingia katika maji ya Iran na kulenga ndege ya abiria ya Shirika la Iran Air, na kuua abiria 290 ambao wote walikuwa ni raia wakiwemo wanawake na watoto. Sio tu kwamba Marekani haikuomba msamaha kwa kitendo hicho, bali pia ilimtunukia medali ya heshima kamanda wa meli hiyo.

Ni dhahiri kuwa, ijapokuwa hatua za  uhasama wa Marekani dhidi ya Iran zimeendelea katika miaka ya hivi karibuni kwa kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vilivyo kinyume cha sheria na hata kuchochea vitendo vya kigaidi dhidi yake, ikumbukwe kwamba ushahidi na nyaraka za kihistoria zinaonyesha wazi kwamba Iran, hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ilikuwa  mlengwa mkuu wa njama na uadui wa maadui, ikiwemo Marekani.