Main Title

source : Parstoday
Jumapili

5 Novemba 2023

17:50:02
1408811

Raisi: Vita dhidi ya Hamas ni sawa na vita dhidi ya demokrasia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria nafasi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) katika uongozi wa serikali halali katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kuwa, vita dhidi ya kundi hilo la muqawama ni sawa na vita dhidi ya demokrasia.

Rais Ebrahim Raisi amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre na kuongeza kuwa, Tehran inakaribisha msimamo wa Oslo wa kutaka kusimamishwa mara moja mauaji dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza, sanjari na kufanyika jitihada za kimataifa za kuliondolea mzingiro eneo hilo, na kuwafikisha misaada ya kibinadamu wakazi wake.

Aidha Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Sheria ya Norway kuchunguza jinai zilizofanywa na Israel huko Gaza na kuongeza kuwa, jinai za kivita za utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani katika eneo hilo hazifai kupita hivi hivi bila kuadhibiwa.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, "Hamas ni serikali halali na iliyochaguliwa kisheria huko Gaza. Vita dhidi ya Hamas ni vita dhidi ya demokrasia."Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, mauaji ya watu zaidi ya 10,000 wakiwemo watoto 4,000 katika Ukanda wa Gaza yametokana na hatua ya Marekani ya kuwamininia Wazayuni shehena za silaha. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Norway amesema nchi yake inafahamu nafasi muhimu na athirifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi. Kadhalika Jonas Gahr Store amepongeza na kusifu juhudi za Iran katika kujaribu kupunguza misiguano na taharuki katika eneo, na vile vile ametoa mwito wa kushirikiana nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu katika kupatia ufumbuzi kadhia ya Palestina. 


/342