Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

9 Novemba 2023

17:23:54
1410089

Netanyahu akataa ombi la Biden la kusitisha mapigano kwa siku 3 huko Gaza

Rais Joe Biden wa Marekani amemtaka Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel asitishe mapigano kwa siku tatu ili kutatua suala la mateka. Kuhusiana na jambo hilo, Biden amesema katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika siku ya Jumanne alimuomba Benjamin Netanyahu asitishe mapigano ili kuandaa uwanja wa kushughulikiwa suala la mateka wa Israel.

Maafisa wa Marekani na Israel wamesema Rais Biden amesema kusimamishwa vita kwa siku tatu kunaweza kusaidia kuachiliwa huru baadhi ya mateka  huko Gaza lakini Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel amekataa ombi hilo. Katika radiamali kuhusiana na upinzani wa Marekani wa kukaliwa tena eneo la Gaza, Netanyahu amesema: 'Mimi sijui kitakachotokea baada ya kuondolewa Hamas, lakini mapigano hayatakomeshwa ila kwa kuiangamiza Hamas.' Huku akitilia mkazo kuendeleza vita Netanyahu  amesisitiza kwamba Wazayuni wanahitajia subira ili kufikia lengo lao la kuiangamiza Hamas, na kuwa hawataki ushindi  nusu.

Upinzani wa wazi wa Netanyahu dhidi ya ombi la Biden la usitisha vita kwa muda wa siku tatu unaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni hauthamini hata mshirika wake wa karibu yaani Marekani, na unawatumia Wamarekani kwa ajili ya kufikia malengo yake katika ardhi za Wapalestina. Katika hali ambayo Biden alisafiri Palestina inayokaliwa kwa mabavu mwanzoni mwa vita na wakati ambapo Tel Aviv ilikuwa ikishambuliwa kwa maroketi ya Hamas kwa ajili ya kutangaza uungaji mkono wake wa dhati kwa Netanyahu na dhamira ya Washington ya kuilinda Israel, lakini waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni hayuko tayari kukubali hata ombi dogo tu la Rais wa Marekani la kusitisha mapigano kwa siku tatu ili kuandaa uwanja wa kuachiliwa huru mateka wake.Inaonekana kuwa suala hili linaweza kuwa chanzo cha mzozo mpya kati ya Biden na Netanyahu. Uhusiano kati ya viongozi  hao umekuwa baridi tangu Biden aingie Ikulu ya White House, na rais wa Marekani amekuwa akijizuia kumualika Netanyahu kwa ajili ya mazungumzo ya  pande mbili. Hatimaye, viongozi  hao walikutana kando ya kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 20 Septemba. Ingawa wanasiasa hao wanafahamiana kwa muda mrefu, lakini wamekuwa na uhusiano mgumu baada ya Biden kuingia Ikulu. Biden amekuwa akiikosoa mara kwa mara serikali ya Netanyahu ya mrengo wa kulia. Hatua ya Joe Biden kutomwalika rasmi Netanyahu katika Ikulu ya White House imeonyesha kutoridhishwa kwa serikali ya Marekani na siasa za baraza la mawaziri la Netanyahu, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya mahakama. Aidha serikali ya Biden huko nyuma ilikosoa upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 1967, lakini kiutendaji haijachukua hatua wala mashinikizo yoyote dhidi ya Tel Aviv ili kusimamisha upanuzi huo.

Pamoja na hayo, ikumbukwe kuwa uhusiano wa Marekani na Israel ni uhusiano wa kistratijia na Washington daima imekuwa ikionekana kuwa muungaji mkono asiye na masharti kwa utawala wa Kizayuni. Aidha, tangu kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na mashambulizi yaliyofuata katika Ukanda wa Gaza, ambayo yamesababisha mauaji ya zaidi ya watu 10,000 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 24,000, utawala wa Biden umekuwa ukiutumia utawala ghasibu wa Israel kiasi kikubwa cha silaha kwa ajili ya kulipua Ghaza. Sasa, katika hatua mpya, Washington inapanga kuutumia utawala huo wa kigaidi mabomu yenye thamani ya dola milioni 320 kwa ajili ya kuwaua kwa umati Wapalestina. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha Wazayuni kuua watu wengi zaidi kadiri inavyowezekana katika Ukanda wa Ghaza.



342/