Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

11 Novemba 2023

17:39:45
1410627

Kikao cha ECO na sisitizo la kusimamishwa mashambulizi ya Israel Ukanda wa Ghaza

Waziri Mkuu wa Pakistan, Anwaar-ul-Haq Kakar amesema katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) kilichofanyika Tashkent, mji mkuu wa Uzbekistan kwamba, tuna wajibu wa kuziunga mkono juhudi za kukomeshwa mashambilizi na jinai za kivita za utawala wa Kizyauni huko Ukanda wa Ghaza.

Waziri Mkuu huyo wa Pakistan amelaani jinai za Israel katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) ina wajibu wa kusaidia juhudi za kukomeshwa haraka jinai na mashambulio ya kikatili ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

Ali Sharif Nejad, mtaalamu wa masuala ya kikanda na kieneo anasema: "ECO inaundwa na nchi muhimu kama Iran, Uturuki, Pakistan na Uzbekistan ambazo kama zitaunganisha nguvu na misimamo yao bila ya kutetereka, zinaweza kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe mashambulizi yake huko Ghaza. Misimamo mizuri sana ya Tehran, Ankara na Islam Abad ya kulaani jinai za Wazayuni na kusisititizia udharura wa kusimamishwa vita haraka, bila ya shaka inachukuliwa kwa msingi huo huo."

Akizungumza kwenye kikao cha 16 cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO huko Tashkent, Uzbekistan, Waziri Mkuu wa Pakistan pia amesema, wale wanaojifanya kuwa eti ni wafuasi wa Nabii Musa AS, wanaelewa vyema kwamba, wao ni wafuasi wa Firauni, si wafuasi wa Nabii Musa; kwa sababu wanafanya jinai za kutisha huko Ghaza. Waziri Mkuu huyo wa Pakistan, Anwaar-ul-Haq Kakar amesema, kwa mtazamo wake, jumuiya ya ECO ina wajibu wa kusaidia juhudi za kusitishwa vita haraka katika Ukanda wa Gahza na ifanye juhudi za pamoja za kuushinikiza utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake na pia kuhakikisha sheria zinafuata mkondo wake dhidi ya viongozi wa Israel kwa jinai zao zote za kivita.

Jinai za utawala wa Kizayuni zinafanyika dhidi ya wananchi madhlumu wa Ghaza kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, madola ya kikatili na kibeberu ambayo hadi hivi sasa yanaendelea kukwamisha juhudi za kusimamisha vita. Katika upande wa pili, wananchi madhlumu wa Ghaza wanaendelea na muqawama wao wa kishujaa huku wakiungwa mkono na watu walio wengi duniani, nchi za Kiislamu na taasisi za kieneo.

Morteza Haidar, mtaalamu mwingine wa masuala ya kimataifa anasema: "Hali ya Ghaza ni mtihami muhimu sana kwa vyama, taasisi na makundi tofauti ya kieneo. Hali hiyo inatoa funzo kwamba, taasisi hizo lazima ziimarishe ushirikiano baina yao na zishikamane vilivyo katika kukabiliana na jinai za Wazayuni na kuhakikisha vita vinasimamishwa haraka huko Ghaza. Kama mshikamano huo utakosekana, basi Wazayuni watazidi kuwa kichwa ngumu na watashadidisha jinai zao dhidi ya watu wasio na hatia." 

Katika upande mwingine, sisitizo la Rais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan kwenye kikao cha ECO cha mjini Tashkent aliyehimiza kuundwa nchi huru ya Palestina linaonesha kuwa, licha ya kupita zaidi ya miongo 7 ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina kunakofanywa na Wazayuni, lakini bado malengo matukufu ya Wapalestina yako hai, na kizazi kipya cha taifa hilo ambacho Wazayuni walikuwa wanaota kwamba kizazi hicho cha Wapalestina kingeisahau na kuidharau ardhi yao ya jadi, bado kiko imara na kinaungwa mkono na walimwengu na nchi nyingi duniani. Tunaweza kusema kuwa, jinai za kuchupa mipaka zinazofanywa na Wazayuni hivi sasa dhidi ya Wapalestina zinatokana na hamaki zilizogubika nyoyo za makatili hao hasa kwa kuona kuwa hivi sasa uungaji mkono wa kadhia ya Palestina umeongezeka zaidi na zaidi sambamba na kuzidi kufedheheka Wazayuni watenda jinai mbele ya walimwengu.

Vilevile, hatua ya Rais Recep Tayyi Erdogan wa Uturuki ya kuilamu vikali Marekani na madola ya Magharibi kwa kushiriki kwao kwenye jinai za Ghaza; pia ni uthibitisho wa ba jinsi ulimwengu ulivyobadilika hivi sasa kwa manufaa ya Wapalestina na dhidi ya utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wa utawala huo katili kama Marekani na madola ya Magharibi.

Katika kikao hicho cha ECO huko Tashkent, Rais wa Uturuki aligusia kuuliwa maelfu ya watu wasio na hatia hasa wanawake na watoto wadogo huko Ghaza na mchango wa madola ya Magharibi kama Marekani kwenye jinai hizo akisisitiza kuwa, asilimia 73 ya zaidi ya watu 11,000 waliouwa kidhulma kwenye mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Ghaza ni wanawake na watoto wadogo na kwamba, jamii ya kimataifa, ina wajibu wa kuchukua hatua haraka za kukomesha jinai hizo.

342/