Hayo yameripotiwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ambalo limeongeza katika taarifa yake kwamba takriban watu 700 wameripotiwa kuuawa, 100 walijeruhiwa na wengine 300 wamepotea katika Jimbo la Darfur Magharibi baada ya kuzuka mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mapigano hayo ni yale ya siku mbili za Novemba 4 na 5 yaliyotokea kwenye eneo la El Geneina huko magharibi mwa Sudan. Ripoti nyingine zimeonyesha idadi tofauti na hiyo ya wahanga wa mapigano hayo kati ya majenerali wa kijeshi huko Sudan.
Kwa upande wake, Shirika la Haki za Kibinadamu la Al-Juzoor ambalo ni shirika la ndani ya Sudan linalotetea haki za binadamu, lilitangaza juzi Alkhamisi kwamba watu 1,300 waliuawa na zaidi ya 2,000 kujeruhiwa katika eneo la Ardamata huko El Geneina yalipozuka mapigano baina ya pande hizo hasimu. Kikundi kingine cha haki za binadamu kilitangaza jana Ijumaa kwamba karibu watu 2,000 wameuawa na wengine 3,000 wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo.
Kuhusu suala hilo, timu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan kwa kifupi UNITAMS imeandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba umepokea taarifa za kusikitisha kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika kwamba kuanzia Novemba 4 hadi 6, baada ya vikosi vya RSF kuchukua udhibiti wa maeneo mbalimbali ya Darfur Magharibi, kulifanyika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kutoka pande zote mbili hasimu, hasa katika kitongoji cha Ardamata cha mji wa El Geneina.
342/