Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

13 Novemba 2023

19:34:05
1411246

Raisi katika mazungumzo na Al-Sisi: Misri ifungue kivuko cha Rafah kwa ajili ya misaada kwa watu wa Gaza

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwambia mwenzake wa Misri, Abel Fattal Al Sisi kwamba, matarajio ya jumla ni kwamba kivuko cha Rafah kifunguliwe ili misaada ya kimataifa iweze kuingia Ukanda wa Gaza.

Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Misri, Abed Fattah Al Sisi kandokando na mkutano wa viongozi wa nchi za Kiislamu na Kiarabu uliofanyika jana mjini Riyadh, Saudi Arabia, kujadili hali ya watu wanaoendelea kuuawa kwa mashambulizi ya Israel wa Ukanda wa Gaza.  

Sayyid Ebrahim Raisi ameongeza kwa kusema: Ni wazi kwa kila mtu kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wanazuia kufunguliwa kivuko cha Rafah kwa ajili ya kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa watu wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Gaza lakini vikwazo hivyo lazima viondolewe.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu Rais amekutaja kufanyika mkutano wa amani wa Cairo kuwa ulikuwa ubunifu mzuri ambao nchi za Magharibi zilizuia kufanikiwa kwake. Ameongeza kuwa: Mkutano wa amani wa Cairo ungeweza kuwa hatua muhimu ya kuhitimisha jinai zinazofanywa na Wazayuni katika mauaji ya wanawake na watoto wasio na ulinzi na wasio na hatia wa Gaza, lakini nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni, zimezuia mafanikio ya mkutano huo, kama ambavyo hazikuliruhusu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na na mashirika mengine ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha uhalifu huu.

Rais Ebrahim Raisi pia amesisitiza ulazima wa kuungana na kushikamana nchi za Kiislamu na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina kikwazo chochote katika kupanua uhusiano na nchi rafiki ya Misri. 

Kwa upande wake, Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi, ameeleza kuwa Cairo ina irada ya uhakika ya kisiasa ya kuanzisha uhusiano halisi na Iran, na akasema: "Kwa sababu hiyo, tumewapa kazi mawaziri husika kuendeleza uhusiano wa kina baina ya nchi hizo mbili." 

342/