Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

17 Novemba 2023

19:36:23
1412502

Jibu la Iran kuhusu kupasishwa azimio la Canada dhidi yake

Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imepitisha azimio jipya kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran katika hali ambayo idadi ya walioliunga mkono ilikuwa ndogo kuliko ya wale waliolipigia au kujizuia kupiga kura.

Azimio lililopendekezwa na Canada dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilipitishwa Jumatano na Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilipasishwa kwa kura 80 za ndio, kura 29 za hapana na nchi 65 zilijizuia kupiga kura. Kwa hakika, nchi 94 hazikukubaliana na azimio hilo. Azimio hilo lilihusiana na machafuko ya mwaka jana nchini Iran ambapo ilidaiwa kuwa haki za wanawake zinakiukwa nchini.

Nukta nyingine ni kuhusu Canada ambayo kila mwaka hupendekeza maazimio kama hayo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Canada ni nchi ambayo ina rekodi nyeusi katika uwanja wa haki za binadamu. Tume Kuu ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kujibu hatua hiyo ya Canada na kutangaza kuwa, mwaka 2021 zaidi ya kesi 34,200 za ubakaji ziliripotiwa nchini humo, jambo ambalo linaonyesha ongezeko la asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.Takriban asilimia asilimia 50 ya wanawake wanaozuiliwa katika magereza ya Canada ni wanawake wa makabila ya wenyeji asilia ambao hutumikia vifungo vya muda mrefu wakiwa katika seli za mtu mmoja mmoja ambapo hupitia kipindi kigumu kabla ya kuachiliwa huru. Asilimia 27.3 ya watu wasio na makazi nchini Canada pia ni wanawake. Kila usiku, wanawake 6,000 (mara nyingi wakiwa na watoto) hutafuta hifadhi katika makazi ya dharura. Asilimia 96 ya wanawake wasio na makazi hupitia aina fulani ya unyanyasaji wa kijinsia, wizi, matusi na vitisho.

Hatua ya Canada na nchi za Magharibi katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imechukuliwa dhidi ya Iran katika hali ambayo walimwengu kwa zaidi ya siku 42 sasa wanashuhudia mauaji ya kimbari na jinai za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa watoto na wanawake wa Gaza. Pamoja na hayo, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na nchi za Magharibi kuhusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea kufanywa na Wazayuni watendajinai huko Gaza ni kana kwamba utawala wa kigaidi wa Israel una kinga ya kisheria kuhusiana na jinai hizo.

Taarifa ya Tume Kuu ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pia inaeleza kwamba, inasikitisha kuona kwamba suala la haki za binadamu sasa linatumika kisiasa kuliko wakati mwingine wowote, ambapo undumakuwili na ubaguzi umekithiri katika uwanja huo. Kuenea jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, ambalo ni dhihirisho la wazi la jinai dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari na  kijamii, kwa upande mmoja, kunaonyesha kutofaulu mikakati ya kutetea haki za binadamu na kwa upande wa pili kunaonyesha wazi siasa za ubaguzi na upendeleo zinaozotekelezwa na mdola makubwa duaniani.Wanaodai kutetea haki za binadamu ambao ndio waanzilishi na waungaji mkono wa michakato eti ya kutetea haki za binadamu na ambao wanapitisha azimio ya mara kwa mara dhidi ya nchi huru kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, si tu kwamba wenyewe wanakabiliwa na mifano ya wazi ya ukiukwaji mkubwa  wa haki za binadamu katika nchi zao, bali sasa wanashirikiana bega kwa bega na utawala wa kibaguzi wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia hasa wanawake na watoto.

Zahra Ershadi, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia amesema kama ifuatavyo katika hotuba yake katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa: Tuelekeze mazingatio yetu kwa nchi za Canada, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel - wahusika wakuu wa ukiukaji wa haki za binadamu na watuhumiwa wa kawaida! Canada na waungaji mkono wa azimio hili wanalipigia kura azimio hili dhidi ya Iran, huku wao wenyewe wakipiga kura ya kupinga azimio lililotaka kukomeshwa umwagaji damu na mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel! Mkanganyiko huu kwa hakika unaonyesha wazi undumakuwili wao kuhusu suala zima la haki za binadamu. Huenda wakati umefika wa kuunda kundi la marafiki wanaounga mkono uchinjaji wa watoto!


342/