Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

18 Novemba 2023

15:28:31
1412809

Safari ya Rais wa China nchini Marekani

Rais Xi Jinping wa China amesisitiza katika mazungumzo yake na Rais Joe Biden wa Marekani katika mji wa San Francisco katika jimbo la California kwamba Beijing na Washington zinapasa kufanya juhudi za kutatua hitilafu kubwa zilizopo baina yao, kila upande uheshimu mistari myekundu na kanuni za upande wa pili na zijiepushe na hatua za kichochezi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Xi Jinping amesema anataraji kuwa Marekani itaiondolea China vikwazo vya upande mmoja na kuandaa anga nzuri ya kibiashara kwa ajili ya makampuni ya Kichina. Hata kama kwa mtazamo wa Beijing, ziara ya Xi huko Marekani na mazungumzo kati yake na Biden lilikuwa jambo la kawaida lakini viongozi wa Marekani wamefanya juu chini kuidhihirisha ziara hiyo kuwa tukio muhimu na kubwa sana katika uhusiano wa pande mbili; na bila shaka Wademocrat wanaoongoza White House nchini Marekani pia wanajaribu kuitumia vibaya kisiasa ziara hiyo. Hii ni kwa sababu inaonekana kuwa Marekani ambayo inajiona kuwa dola kuu lenye nguvu duniani limeshindwa kuyapatia ufumbuzi matatizo mengi ya kimataifa. Aidha kwa kupuuza nafasi ya China katika kusogeza mbele mipango ya kikanda na kimataifa ukiwemo mgogoro wa Ukraine, Marekani inahitaji kushirikiana na kuelewana na China kwa sababu nchi za Magharibi khususan Marekani zimenasa katika kinamasi cha mgogoro huo na hazina tena uwezo wa kuendeleza mgogoro wa Ukraine. 

Li Su Xuan mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia suala hilo kwa kusema: Joe Biden ni kama mtu ambaye alihitajia pakubwa kukutana na Xi Jinping ili kujiondoa katika mkwamo huo; na kwa msingi huo duru za kisiasa zenye mfungamano na serikali ya Marekani na chama cha Democrat ziliakisi pakubwa ziara ya Rais wa China kabla na baada ya kuelekea Marekani. Duru hizo zimejaribu pakubwa kuionyesha ziara hiyo kuwa mafanikio na muhimu kwa Biden.  Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, katika mazungumzo hayo, Rais wa China amemweleza Biden nukta muhimu kuhusu hisia za China katika uga wa kibiashara na kiuchumi na kusisitiza kuwa, suala la Taiwan ni nukta muhimu kwa Beijing, na kwamba Washington haipasi kuihepa kwa kuzingatia hamu kuu ya Biden ya kutaka kukutana na kufanya naye mazungumzo. Wakati huo huo baadhi ya wachambuzi wa mambo hawapingi kwamba Biden amedhihirisha msimamo huo katika fremu ya sera za Washington za kuamiliana na nyenendo za Beijing kwa sababu hatua za karibuni za kijeshi na kisiasa za Marekani dhidi ya China zimeikasirisha nchi hiyo na hivyo kuzidisha mwanya kati ya Washington na Beijing. Kwa mtazamo wa Washington, kuendelea hali hii kunaweza kuzuia ushirikiano wa dunia na Beijing kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali  ya kikanda na kimataifa.  

Su Shu Hiswan mchambuzi wa masuala ya kimataifa anasema kuhusiana na hilo kwamba: China inafahamu vyema kuwa Washington haiheshimu wala kufungamana na ahadi na wajibu wake kuhusu China bali zaidi inatekeleza hatua za kimaonyesho tu mkabala wa Beijing; ambapo lengo kuu ni kujaribu kuidhibiti China na maamuzi yake katika hali ambayo China inadhihirisha kivitendo kuwa inafanya kazi kwa uhuru kabisa na katika fremu ya kulinda maslahi yake.  

Al kul haal, msimamo wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China wa kulaani matamshi ya Rais wa Marekani ambaye kwa mara nyingine tena amemtaja rais wa nchi hiyo kuwa dikteta unaonyesha kutobadilika msimamo wa Marekani kuhusu China, huku Marekani ikiitambua China kuwa hasimu wake mkuu asiyeweza kudhibitiwa.

Kwa msingi huo haionekani kuwa licha ya taarifa zilizoenea kuhusu mazungumzo chanya na yaliyozaa matunda kati ya Biden na Xi, mazungumzo ya wawili hao hayana athari katika kubadili mwelekeo na hatua za Marekani mkabala wa China. Hii ni katika hali ambayo China inaendelea kusisitiza juu ya kuendelea na ushirikiano unaofungamana na ushindani na Marekani. Kwa kuwa Rais wa China ameelekea Marekani kwa lengo la kushiriki katika Mkutano wa Asia- Pacific Economic Cooperation (APEC) huko Francisco; inaonekana kuwa mazunumzo kati yake na Biden yalipangwa tokea awali. 


342/