Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

11 Desemba 2023

14:33:10
1419338

Msimamo imara wa wananchi na vyama vya Uturuki kuhusu uhusiano na Israeli na uwepo wa Marekani huko Incirlik

Kufuatia kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wa Gaza na uungaji mkono mkubwa wa Marekani kwa jinai hizo, wananchi wa Uturuki wamefanya maandamano mjini Istanbul na kutoa matakwa mapya kwa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan.

Wananchi wa Uturuki kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano dhidi ya Israel, Marekani na dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza. Huku wakilaani mashambulizi yasiokuwa na kikomo ya utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake katika Ukanda wa Gaza na kuonyesha uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina, waandamanaji wametaka kusimamishwa uuhusiano na ushirikiano wa aina yoyote ile wa kibiashara na kisiasa kati ya Uturuki na utawala ghasibu wa Israel. Wakati wa maandamano hayo makubwa, Dogu Princek, kiongozi wa Chama cha Uturuki cha Kitaifa, ametaka kuondoka mara moja kwa wanajeshi wa Marekani kutoka katika Kambi ya Anga ya Incirlik. Mwanasiasa huyo wa Uturuki ameelezea udharura wa kuondoka jeshi la anga la Marekani katika Kambi ya Anga ya Incirlik na kutaka kukabidhiwa kambi hiyo kwa Jeshi la Anga la Uturuki. Mwanasiasa huyo amesema:

Udharura wa kuondoka vikosi vya Marekani katika Kambi ya Anga ya Incirlik kusini mwa Uturuki ni wa historia na Chama cha Kitaifa kinataka kukabidhiwa udhibiti wa kituo hicho kwa Jeshi la Anga la Uturuki.

Hivi karibuni Wizara ya Ulinzi ya Uturuki ilithibitisha kupelekwa silaha za Marekani Israel  kupitia kambi ya Incirlik. Hivi sasa kituo cha anga cha Incirlik kilichoko mkoa wa Adana kusini mwa Uturuki kinatumiwa na Jeshi la anga la Marekani. Jeshi la Marekani pia linadhibiti kituo cha rada cha kutoa onyo ya mapema ya mashambulizi ya makombora katika eneo la Kurecik katika mkoa wa Maltiye kusini mashariki mwa Uturuki, ambacho kinachukuliwa kuwa sehemu ya mfumo wa ulinzi wa makombora wa Umoja wa NATO. Hivi sasa ukweli huu uko wazi zaidi kwamba wanasiasa wanaotawala Uturuki, kwa upande mmoja, wanajionyesha kuwa ni watetezi wa watu wa Palestina, haswa wakaazi wa Gaza, lakini kwa upande mwingine, wanaendeleza biashara kubwa na kushirikiana kiuchumi na utawala wa Kizayuni. Ni kwa sababu hiyo, ndipo viongozi wa serikali ya Recep Tayyip Erdoğan wametuhumiwa na baadhi ya nchi na hata raia wa Uturuki yenyewe kuwa wanatekeleza siasa za kuuma na kupuliza.Viongozi wa Uturuki wanatelekeza siasa za kundumakuwili kwa kuiuzia Israel bidhaa za kimkakati kama vile mafuta, gesi na chuma na wakati huo huo kudai kutetea kadhia ya Palestina na wananchi madhulumu wa Gaza. Hii ni licha ya ukweli kuwa katika muda wa chini ya miezi miwili, zaidi ya wakazi 17,900 wa Gaza wameuawa shahidi na zaidi ya 46,000 kujeruhiwa. Licha ya kuwa wengi wa mashahidi na majeruhi hao wa Palestina ni raia, lakini utawala wa kibaguzi wa Israel bado unaendeleza mauaji yake ya halaiki katika ukanda huo. Kufuatia kufanyika maandamano makubwa dhidi ya Marekani na Israel nchini Uturuki, Devlet Bahçeli mshirika wa Recep Tayyip Erdogan katika muungano unaojulikana kwa jina la Jumhuri ametoa masharti mapya kwa Uswisi kwa ajili ya kujiunga na Shirika la Umoja wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO). Hii ni pamoja na kuwa, viongozi ya Uturuki, haswa Erdoğan, hadi sasa wamekuwa wakitoa masharti mengi kwa Sweden ili iweze kupata uanachama katika shirika la kijeshi la NATO. Hata hivyo, hakuna masharti yoyote ya Uturuki yaliyokubaliwa na nchi zinazotafuta uanachama wala viongozi wa shirika hilo la kijeshi. Kupambana na Chama cha Kurdistan cha Uturuki (PKK), kukabiliana na wanaopinga Uislamu na kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu pamoja na kukubaliwa uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa masharti yanayotolewa na Uturuki kabla ya kukubali uanachama wa Uswisi katika NATO, ambapo hakuna hata moja ya masharti hayo lililokubaliwa na nchi za Magharibi.



342/