Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

14 Desemba 2023

15:47:39
1420243

Kutokuwa na nia nchi za Magharibi kuipa Uturuki uanachama katika Umoja wa Ulaya

Huku serikali ya Uturuki ikiwa imeanzisha juhudi mpya za kujiunga na Umoja wa Ulaya, matokeo ya kura mpya ya maoni yanaonyesha kuwa raia wengi wa Ulaya wanapinga nchi hiyo kupewa uanachama katika umoja huo.

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Baraza la Ulaya kuhusu Mahusiano ya Kigeni (ECFR) yanaonyesha kuwa ni idadi ndogo tu ya raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaounga mkono Uturuki kujinga na umoja huo. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni upinzani wa mataifa ya Ulaya ya Kati na Mashariki kwa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, raia wengi kati ya asilimia 60 hadi 65 wa Poland na Romania wanapinga Uturuki kujiunga na umoja huo. Hii ni katika hali amabyo, raia wa Bulgaria, Poland na Romania, husafiri Uturuki kila siku kwa ajili ya kununua bidhaa wanazohitaji kutokana na unafuu wa bei ya bidhaa hizo nchini humo kufuatia kushuka kwa thamani ya sarafu yake ya kitaifa.

Jambo la kushangaza ni kwamba serikali na raia wa nchi hizo muongo mmoja uliopita, walionyesha nia yao ya kuiruhusu Uturuki ijiunge na Umoja wa Ulaya. Mataifa ya Ulaya ya Kati yanapinga Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, huku kundi jingine kubwa la raia wa Austria, Ujerumani, Ufaransa na Denmark wakipinga pia nchi hiyo kujiunga na umoja huo. Tangu 1964, serikali ya Ankara imekuwa ikijaribu kuwa nchi ya Ulaya, jambo ambalo limeipelekea kufanya mageuzi makubwa katika sheria na utamaduni wake ili kufikia lengo hilo.Licha ya juhudi za takriban miaka 70 ambazo zimefanywa na wanasiasa wa Uturuki katika uwanja huo, lakini hawajafanikiwa kujiunga na Umoja wa Ulaya na hii ni pamoja na kuwa nchi hyo imeruhusiwa kujiunga na baadhi ya taasisi muhimu za umoja huo kama vile Umoja wa Forodha wa Ulaya. Hii ina maana kwamba serikali za Ulaya zina lengo la kunufaika na fursa za huduma na bidhaa za bei nafuu za viwanda vya Uturuki licha ya kuinyima nchi hiyo uanachama katika Umoja wa Ulaya. Siasa hizo za serikali za Magharibi zimekuwa wazi kabisa katika miongo saba iliyopita hivi kwamba baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wa Uturuki wanauchukulia Umoja wa Ulaya kuwa klabu maalumu ya Wakristo.

Bibi Dorothe Schmidt, mtafiti na mkuu wa ratiba ya Uturuki ya Kisasa katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Ufaransa na mchambuzi mashuhuri wa taasisi hiyo, alisema hivi muongo mmoja uliopita: "Neno "klabu ya Kikristo" linatumiwa zaidi na wanasiasa na wachambuzi wa Uturuki. Kwa kweli, dini haijaashiriwa popote katika katiba ya Umoja wa Ulaya. Pamoja na hayo suala hilo linajadiliwa katika fikra za waliowengi katika Umoja wa Ulaya. Hii leo, kura za maoni zinaonyesha kuwa ni asilimia 30 pekee ya raia wa Ulaya ndio wanaunga mkono Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya."

Kwa upande mwingine, hatupaswi kupuuza ukweli kwamba viongozi wa serikali ya Uturuki, baada ya vita vya maneno na serikali za Ulaya katika miongo miwili iliyopita, hivi karibuni wamefungua njia mpya ya kukaribiana na kuimarisha uhusiano wao na nchi za Ulaya. Hatua ya hivi karibuni ni ile iliyochukuliwa na serikali ya Uturuki ya kutengeneza daraja juu ya bahari kati ya nchi hiyo na Ugiriki ili magari yaweze kusafiri kwa urahisi zaidi kati ya nchi mbili. Serikali ya Uturuki pia inajaribu kuimarisha uhusiano wake na baadhi ya nchi nyingine zenye nguvu za Umoja wa Ulaya, yaani Ujerumani, Ufaransa na Italia.

Hatua hizo za serikali ya Uturuki kwa mara nyingine zimewekwa kwenye ajenda ya kazi katika hali ambayo David Cameron, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, aliwahi kusema: "Uturuki haitaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya hadi mwaka wa 3000."