Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

16 Desemba 2023

12:06:53
1420686

Kushindwa Umoja wa Ulaya kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu mgogoro wa vita vya Gaza

Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Ulaya umemalizika huku viongozi wa nchi 27 za Ulaya wakishindwa kufikia makubaliano ya pamoja katika taarifa yao ya mwisho kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na matukio ya Gaza.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, alisema wazi Ijumaa jioni katika kikao na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa baraza hilo kwamba: 'Tumeshindwa kufikia msimamo wa pamoja na jumuishi kuhusu matukio ya Gaza.'

Hata hivyo, Charles Michel, Rais wa Baraza la Ulaya amejaribu kuficha hitilafu za ndani za Umoja wa Ulaya kuhusu Palestina kwa kurejelea misimamo ya pamoja ya nchi za Ulaya kuhusu suluhisho la "serikali mbili" na pia kulaani jinai za Walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Amedai kuwa madhumuni ya kufanyika mkutano wa duru hii ya mazungumzo hayakuwa kuhusu  taarifa ya mwisho ya matukio ya Gaza, na kwamba msimamo wa baraza hilo kuhusu suala hilo ulitangazwa katika taarifa ya duru iliyopita. Hii ni katika hali ambayo Michel katika barua kwa viongozi wa Ulaya kabla ya kufanyika mkutano huo alisema kuwa matukio ya Mashariki ya Kati yangekuwa moja ya mada muhimu katika ajenda ya mkutano huo. Alisema, wangedai kuachiliwa huru wafungwa wote na kushughulikiwa hali ya kutisha ya kibinadamu huko Gaza. Hii ni katika hali ambayo, taarifa ya mwisho ya baraza hilo, iliashiria kwa sentensi fupi tu hali jumla ya eneo kwa kusema: 'Baraza limejadili kwa kina masuala ya kimkakati kuhusu Mashariki ya Kati.'

Misimamo tofauti ya viongozi wa Ulaya kuhusu  vita vya Gaza inatokana na mitazamo tofauti ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala la Palestina. Baadhi ya nchi kama vile Uhispania, Ireland na Ubelgiji zinataka kutambuliwa wazi taifa la Palestina na zimelaani  jinai za utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza. Hii ni katika hali ambayo waitifaki wa  Marekani barani Ulaya kama vile Ujerumani na Austria na nchi za Ulaya Mashariki kama vile Jamhuri ya Czech wanaiunga mkono Israel na wanataka kuendelea operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza. Kama ilivyoshuhudiwa katika upigaji kura wa azimio la karibuni la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu usitishaji vita Gaza, Austria na Jamhuri ya Czech pamoja na Marekani zilipiga kura dhidi ya azimio hilo. Bila shaka, Ufaransa imechukua msimamo wa kati na kwa kuunga mkono eti haki ya Israel ya kujilinda, na hatua zake katika Ukanda wa Gaza,  katika baadhi ya misimamo yake, imetoa wito wa kukomeshwa mauaji ya raia wa Palestina. Ikiwa nchi muhimu ya Ulaya ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Uingereza pia  sambamba na Marekani, viongozi wa Ujerumani na Ufaransa, imepinga usitishaji vita huko Gaza hadi pale Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas itakapoangamizwa. Tofauti za misimamo kati ya nchi za Ulaya zimepelekea Baraza la Ulaya kushindwa kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu vita vya Gaza, hasa ombi la kusitishwa mapigano katika vikao vyake vya hivi karibuni.Suala hilo limezua shutuma nyingi ndani ya Ulaya. Waziri Mkuu wa Ireland Leo Varadkar ameushutumu Umoja wa Ulaya kwa kushindwa kuwa na msimamo thabiti na wa pamoja kuhusu vita vya Gaza, na kusema Umoja huo umepoteza itibari yake ulimwenguni. Katika hotuba yake kabla ya mkutano wa Baraza la Ulaya, Varadkar alisema kuwa msimamo wa nchi za Ulaya kuhusu mzozo wa Gaza umebadilika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita na kukaribiana na msimamo wa muda mrefu wa Ireland katika kuunga mkono Palestina na kusema: 'Nitawasisitizia viongozi wa Ulaya kuwa umoja huo umepoteza itibari kutokana na kutokuwa na msimamo thabiti kuhusiana na mzozo wa Palestina na Israel. Pia tumepoteza satwa kwa sababu ya kile kinachoonekana kuwa ni siasa za undumakuwili, jambo ambalo si madai yasiyo na maana.' Waziri Mkuu wa Ireland ameongeza: 'Tunahitaji kuwa na sauti moja katika taarifa ya mwisho, ili pamoja na kulaani ugaidi, tuwe na wito mmoja wa kusitisha vita kwa ajili ya ubinadamu (huko Gaza) na kuwepo na uadilifu kuhusu Wapalestina chini ya kivuli cha suluhisho la serikali mbili.' Hata hivyo, taarifa ya mwisho ya kikao cha Baraza la Ulaya inaonyesha kuwa kukubaliwa ombi la Waziri Mkuu wa Ireland na viongozi wa Ulaya ni jambo lisilowezekana na hilo linatoka na misimamo ya karibu ya baadhi ya nchi za Ulaya na Washington na kwa upande mwingine kuwepo lobi zenye nguvu za Wazayuni barani humo. Kimsingi ni jambo lililo mbali sana kubadilishwa misimamo na kuchukuliwa siasa za kati kutokana na sera za undumakuwili za baadhi ya nchi kuhusiana na kadhia ya utawala wa Kizayuni na Wapalestina.