Main Title

source : Parstoday
Jumanne

19 Desemba 2023

16:17:37
1421656

70% ya vijana wa Ukraine wako tayari kukana uraia wao ili wasipelekwe kupigana vita na Russia

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Ukraine yanaonyesha kuwa zaidi ya 70% ya wanaume nchini humo wako tayari kuukana uraia wao ili waepuke kuhudumu jeshini na kupelekwa kupigana vita na Russia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Mariana Bezohla, Naibu Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge la Ukraine, alitangaza matokeo ya uchunguzi huo wa maoni jana Jumatatu kwenye mitandao ya kijamii.

Kulingana na afisa huyo wa Ukraine, kati ya washiriki 3,773, 74% walitoa jibu la 'ndiyo' kwa swali la uchunguzi huo wa maoni, walipoulizwa kama wangependelea kuukana uraia wa Ukraine mkabala wa kuhepa kwenda kupigana vita na Russia.

Matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni yametolewa wakati vita kati ya Ukraine na Russia vikiwa vinaendelea, huku jeshi la Ukraine likipata hasara ya zaidi ya askari 125,000 waliouawa, ikiwa ni sawa na idadi ya divisheni zisizopungua tano, tangu lilipoanzisha mashambulio wakati wa msimu wa joto kwa lengo la kuyatwaa tena maeneo yaliyotekwa na vikosi vya Russia.

Wakati huo huo, suala la Ukraine kupatiwa misaada zaidi na Marekani limebaki kuwa kitendawili katika Bunge la nchi hiyo, na kuzidi kuitia mashakani hatima ya vita hivyo, ambavyo vinakaribia kutimiza miaka miwili.

Televisheni ya CNN, mtandao wa habari wa Baraza la Atlantiki na gazeti la Economist zimeeleza katika ripoti zao kuwa kukosekana dira ya kimkakati miongoni mwa nchi za Ulaya, kulipa kisogo nchi za Magharibi suala la kuisaidia na kuiunga mkono Ukraine, nguvu za kijeshi za Russia na kuchoshwa na vita vikosi vya jeshi la Kiev ni sababu zinazoipa Moscow matumaini ya kupata ushindi katika vita hivyo.

Sergei Naryshkin, mkurugenzi wa idara ya intelijensia ya nje ya Russia alisema wiki iliyopita kwamba: nchi za Magharibi hatimaye zitaiacha serikali ya Ukraine peke yake.

Vita nchini Ukraine vilianza kutokana na nchi za Magharibi kutojali wasiwasi wa kiusalama iliokuwa nao Moscow na kusambazwa kwa wingi vikosi vya shirika la kijeshi la NATO hadi karibu na mipaka ya Russia.../

342/