Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

21 Desemba 2023

15:07:57
1422311

Mashirika ya kiraia Uhispania yataka kusitishwa biashara ya silaha na Israel

Wanaharakati kutoka mamia ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Uhispania wamefanya maandamano na kukusanyika nje ya Bunge la nchi hiyo wakiitaka serikali yao isimamishe bishara ya silaha na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa Harakati ya Kimataifa ya Kuususia Utawala haramu wa Israel BDS, mamia ya wafuasi na waungaji mkono wa mashirika 375 ya kiraia pamoja na vyama vitano vya kisiasa wameshiriki kwenye maandamano hayo ya kutaka kufutwa mapatano ya silaha baina ya Uhispania na Israel.

Wakati maandamano hayo yakifayika nje ya Bunge mjini Madrid, ndani ya taasisi hiyo ya kutunga sheria, Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez sanjari na kutaka kusitishwa vita Gaza kwa sababu za kibinadamu, amesisitiza kuwa yanayojiri katika ukanda huo ni majanga ambayo hayawezi kustahamilika. 

Pasi na kuashiria chochote kuhusu mashinikizo ya kutaka nchi hiyo isimamishe mauzo ya silaha baina yake na Israel, amesema wakati umefika kwa Ulaya kupaza sauti na kuzungumzia mzingiro dhidi ya Gaza ambao umewazidishia mashaka wakazi wa eneo hilo.

Kiongozi wa chama cha kisiasa cha Podemos, Ione Belarra amemtaka Waziri Mkuu wa Uhispania kutangaza mashambulizi dhidi ya Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari sambamba na kuiwekea Israel vikwazo vya silaha.Oktoba 4, serikali ya Uhispania iliidhinisha mkataba wa kununua makombora 1,680 ya kukabilliana na vifaru kwa thamani ya yuro milioni 285. Ingawaje makombora hayo yanatengenezewa Uhispania, lakini kampuni inayozizalisha ni tawi la shirika la Kizayuni la mifumo ya ulinzi la Rafael. Mwezi mmoja kabla, Uhispania iliidhinisha mkataba wa kununua mifumo ya kuvurumisha maroketi ya SILAM inayotengenezwa na kampuni ya Israel ya Elbit, ambayo pia inazalisha silaha na zana za kivita zinazotumiwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Juzi Jumanne, Manu Pineda, mwakilishi wa Uhispania katika Bunge la Ulaya mbali na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo katika eneo hilo, alitaka Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo haramu apandishwe kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutokana na jinai na mashambulio ya kinyama yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina.

342/