Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

28 Desemba 2023

15:24:11
1424600

SEPAH: Kisasi cha mauaji ya Jenerali Razi Mousavi kitakuwa maangamizi kwa Israel

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) anasema kuwa, kisasi cha Iran kwa jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kumuua kigaidi mshauri mkuu wa kijeshi nchini Syria hakitakuwa chochote bali ni kuutokomeza kabisa utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu.

Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo leo Alhamisi wakati wa maziko ya Brigedia Jenerali Sayyid Razi Mousavi, kamanda wa SEPAH ambaye aliuawa shahidi katika shambulio la anga la kigaidi la Israel katika kitongoji kimoja cha mji mkuu wa Syria, Damascus, siku tatu zilizopita.

Amesema: "Kumuua shahidi Sayyid Razi kunatokana na udhaifu mkubwa wa utawala wa Kizayuni. Hatupotezi muda wowote katika kulipiza mauaji ya watu wetu. Kulipiza kisasi kwa Sayyid Razi hakutakuwa kitu kingine chochote ila kuutokomeza kabisa utawala wa Kizayuni."

Kamanda Salami pia amesema kuwa, Jenerali Mousavi alikuwa ni mmoja wa makamanda wa SEPAH wenye uzoefu na ufanisi mkubwa katika kambi ya muqawama.Ameongeza kuwa, kamanda Mousavi ameuawa shahidi katika njia ile ile ya kupambana na ugaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran SEPA akiongeza kwamba Mousavi hakuwahi kuondoka kwenye uwanja wa jihad kwenye kipindi chote cha miaka 45 iliyopita. Pia amesema: "Mousavi alibaki imara baada ya [mauaji ya] Haj Qassem na amekuwa muda wote pamoja na na [Kamanda wa hivi sasa wa Kikosi cha Quds cha SEPAH Brigedia Jenerali Esmail] Qa'ani. Pia amesema: “Adui alimfahamu Jenerali Razi kuliko sisi kwa sababu alikuwa amepata vipigo vikali kutoka kwake." Leo asubuhi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameongoza Sala ya Maiti ya kuusalia mwili wa Kamanda Shahidi Sayyid Razi Mousavi pamoja na kumsomea Faatiha na kumuombea dua Shahidi huyo. 

342/