Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

29 Desemba 2023

18:19:16
1424805

Khatibu wa Sala ya Ijumaa asisiitiza kudumishwa Hamasa ya tarehe 9 Dey

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesisitiza kudumishwa na kuendelezwa kumbukumbu ya Hamasa ya tarehe 9 Dey.

Kesho Jumamosi, ni siku ya kuadhimisha kumbukumbu ya Hamasa ya tarehe 9 Dey. Tarehe 9 Dey 1388 inayosadifiana na Desemba 30, 2009 inakumbusha maandamano yaliyofanywa na mamilioni ya wananchi wa Iran kutangaza kujibari na kujitenga na wavurugaji nidhamu ya jamii na kutoa jibu madhubuti pia kwa wazushaji fitna, walioamua kufuata njia pogo na isiyo sahihi kwa kisingizio cha kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa kumi wa rais wa Iran. Hamasa ya Dey 9 ni nembo ya heshima, uhuru na basira ya wananchi wa Iran, ambao walisimama imara hata kwa gharama ya kutoa mhanga roho zao kwa ajili ya kulinda usuli na misingi ya Uislamu na malengo matukufu ya Mapinduzi na kupaza sauti zao kwamba ikiwa maadui watasimama dhidi ya dini yao, na wao watasimama dhidi ya ulimwengu wao wote. Kwa mnasaba huo na kwa mujibu wa IRNA, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema katika khutba za Sala ya Ijumaa ya wiki hii hapa Tehran ya kwamba: "hatua makini na subira ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi na kujitokeza kikamilifu wananchi tarehe 9 Dey kuliiokoa Iran na fitna hiyo hatari; kwa hivyo, lazima tuidumishe siku hii na tuwafungie njia wafanya fitna kwa basira na urazini".Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa: "kilichotokea wakati wa fitna ya Marekani ya mwaka 88 Hijria Shamsia ni uadui uliokuwa umepangwa na kuratibiwa na maadui walioikamia Iran ya kwamba, kama hawatafanikiwa kabla ya uchaguzi, wachukue hatua baada ya uchaguzi; na ndio kama mlivyoona, katika mwaka 88 ilitokea fitna hatari zaidi kuwahi kushuhudiwa tokea Mapinduzi".

 Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari amezungumzia pia chaguzi za Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Mkuu na wa Bunge zitakazofanyika mwezi Esfand (Machi mwakani) na kubainisha kuwa: uchaguzi una umuhimu mkubwa sana, ambao ni kuzuia  udikteta na fujo, ambapo katika mtazamo huo wa kimkakati maslahi ya wananchi yanalindwa. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amegusia stratejia nne za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambazo ni ushiriki kwa wingi, ushindani mkubwa, uchaguzi huru na wa haki na kufanyika kwa amani na usalama na akasema: hatua inayopigwa na taifa la Iran kuelekea kwenye vilele vya maendeleo inaendelea, na uchaguzi ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa wananchi wa Iran kwa ajili ya uhuru na kujitawala taifa lao. Katika sehemu nyingine ya khutba zake, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari ameashiria matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyotoa siku ya Jumatano katika mkutano na akina mama na akasema, kuuangamiza utambulisho wa mwanamke na kuuzika ukiwa hai ndizo sifa za ujahilia mamboleo. Mwishoni mwa khutba zake, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria vita vya Gaza na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na akasema: Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kwamba, Wazayuni wote watenda jinai wametenda jinai zao kwa namna ya pekee na isiyo na mfano; na watu wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao pia wameonyesha Muqawama wa namna ya pekee, na wanalipiza kisasi kwa maadui cha miaka 75 ya jinai zao.../