Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

30 Desemba 2023

16:58:45
1425171

Kamanda Qaani: Uhodari wa utawala wa Kizayuni na Marekani ni kuua wanawake na watoto wasio na hatia

Brigedia Jenerali Esmail Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amehoji, ni mafanikio gani ambayo utawala wa Kizayuni na Marekani zimepata tangu zilipoanzisha vita? na akasema: uhodari wao ni kuua wanawake tu na watoto wasio na hatia.

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC ameihutubu Marekani kwa kuiambia: "ikiwa mtaendelea na mwenendo wenu usio na mantiki nchini Iraq, Muqawama wa Iraq utaachana na kutumia busara na kutoa jibu jingine dhidi yenu".

Brigedia Jenerali Qaani amewahutubu pia viongozi wa utawala wa Kizayuni akisisitiza kwa kuwaambia: "mumemuua kigaidi Shahidi Razi Mousavi kwa sababu hamkuweza kupata chochote katika medani ya vita ya Gaza na Iran haitanasa kwenye njama na mipango yenu".

Ameendelea kueleza kwamba leo kila moja kati ya kambi za Muqawama katika eneo ina muundo wake huru na mwafaka, na akabainisha kuwa: makundi ya Muqawama yamestawi hatua kwa hatua na leo hii nguzo zote za kambi ya Muqawama katika ngazi ya kikanda zinapambanua mambo na kujichukulia maamuzi.Kamanda Qaani amefafanua kuwa: katika kipindi hiki pia, Muqawama wa Palestina umeanza kuchukua hatua kwa mipango na mikakati uliojipangia wenyewe, na kwa mara ya kwanza katika kipindi hiki, kutokana na kushamiri jinai kubwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi Waislamu wa Palestina, muqawama huo ulijiandaa na kujipanga, na kutekeleza hatua kwa hatua yale uliyoyafanya, tena vizuri sana na kwa umakini.

Itakumbukwa kuwa tarehe 7 Oktoba 2023, makundi ya Muqawama ya Palestina yalianzisha operesheni ya mashambulio ya Kimbunga cha Al-Aqsa kutokea Ukanda Gaza dhidi ya vituo na ngome za utawala wa Kizayuni; na katika hatua ya kulipiza kisasi, kufidia kushindwa kwake na kutaka kusimamisha operesheni za makundi ya Muqawama, utawala huo ghasibu ukaanzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya maeneo ya makazi na vituo vya tiba na kiutamaduni vya Ukanda wa Gaza, mashambulio ambayo hadi sasa yamepelekea kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina 21,000 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 55,000.

Akthari ya waliouawa katika mashambulio hayo ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel huko Ukanda wa Gaza mbele ya macho ya walimwengu ni wanawake na watoto.../


342/