Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

13 Januari 2024

12:48:26
1429038

Abdollahian: Kama Marekani inataka amani, iache kuunga mkono jinai za Israel

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Marekani inapaswa kuacha mara moja kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni badala ya kufanya mashambulizi nchini Yemen kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kupatikana amani kwenye kona zote za ukanda huu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Amir-Abdollahian amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi kwenye mtandao wa kijamii na kuongeza kuwa, hatua ya Yemen ya kuwaunga mkono wanawake na watoto wa Ghaza mbele ya jinai na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni inapaswa kupongezwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, San'a inaheshimu kikamilifu usalama wa usafiri wa baharini na inachofanya ni kuzuia tu meli za Israel na zinazoshirikiana na utawala wa Kizayuni ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono wanawake na watoto wa Ghaza wanaouliwa kinyama na Israel.Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yamekuja baada ya Marekani na Uingereza kufanya mashambulizo jana Ijumaa na mapema leo Jumamosi dhidi ya maeneo tofauti ya Yemen kwa kutumia makombora 100 na kupelekea watu watano kuuawa na wengine sita kujeruhiwa huko Yemen. Kwa upande wake, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulio ya Marekani na Uingereza nchini Yemen na kusisitiza kuwa mashambulizi kama hayo ya kiholela ni uvunjaji wa wazi wa haki ya kujitawala ardhi ya Yemen na ni ukiukaji wa sheria na haki za kimataifa. Ameelezea wasiwasi wake kutokana na madhara ya mashambulizi hayo kwa usalama na amani ya eneo hili na duniani kiujumla na ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuzuia kuenea vita na ukosefu wa utulivu na amani katika eneo hili.

342/