Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

15 Januari 2024

13:06:48
1429602

"Dunia ina wajibu wa kuunga mkono kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel ICJ"

Mwakilishi wa Slovenia katika Bunge la Ulaya amesema dunia ina jukumu la kuunga mkono kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel, kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Matjaz Nemec alinukuliwa akisema hayo jana Jumapili na shirika la habari la Anadolu na kuongeza kuwa, "Tunachoshuhudia Gaza ni juhudi za maghasibu kuliangamiza taifa."

Ameeleza bayana kuwa: Hakuna anayeweza kuzuia haki ya taifa la Palestina kujiamulia hatima yake, kama ambavyo hakuna anayeweza kutunyima haki hii. Hii ndio maana Slovenia lazima iendelee kushinikiza mchakato wa amani utakaopelekea kutambuliwa taifa huru la Palestina.  

Mbunge huyo wa Bunge la Ulaya amesisitiza kuwa, mashambulizi ya Israel dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza ni mfano wa wazi wa mauaji ya kimbari.

Mwakilishi huyo wa Slovenia katika Bunge la EU amekosoa kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za Israel huko Gaza kwa kusema: Hadi lini Ulaya na dunia zitaendelea kutazama tu taifa likifutwa mbele ya macho yetu?

Hii ni katika hali ambayo, juzi Jumamosi, mamilioni ya watu katika miji na majiji 121 kwenye nchi 45 kote duniani walijitokeza mabarabarani kushiriki maandamano ya kulaani siku 100 za jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza, chini ya kaulimbiu ya "Siku ya Hatua ya Ulimwengu." Walimwengu walioshiriki kwa wingi maandamano hayo walitoa wito wa kusitishwa mara moja vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, vilivyoua shahidi Wapalestina karibu 24,000, aghalabu yao wakiwa ni wanawake na watoto, mbali na wengine zaidi ya 60,000 kujeruhiwa. Mahakama ya ICJ yenye makao yake makuu mjini The Hague nchini Uholanzi hivi karibuni ilianza kusikiliza ombi la Afrika Kusini la kutaka kuchunguzwa tuhuma dhidi ya Israel za kufanya mauaji ya kimbari katika vita vya Gaza.

342/