Main Title

source : Parstoday
Jumanne

16 Januari 2024

18:32:24
1429956

Kuongezeka hitilafu katika serikali ya Biden kuhusiana na vita vya Gaza

Sambamba na uendelea vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu madhulumu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina, kuzidi kuzorota hali ya mambo katika eneo la Magharibi mwa Asia na himaya ya wazi na ya siri ya Marekani kwa utawala huo ghasibu, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa hali inazidi kuwa ngumu kwa Marekani siku baada ya siku kutokana na kuendelea kuunga mkono jinai za Israel, hasa mauaji ya halaiki ya Wapalestina.

Hali hiyo, taratibu, inadhihirisha zaidi migawanyiko na hitilafu katika serikali ya Biden katika uwanja huo.

Katika muktadha huo, tovuti ya Huffington Post imetangaza kujiuzulu kwa David Satterfield, Mjumbe Maalumu wa serikali ya Joe Biden katika masuala ya kibinadamu huko Gaza, jambo ambalo linaakisi kuwepo hitilafu baina ya maafisa wa serikali ya Marekani. Kwa msingi huo, balozi mstaafu ambaye  Rais Joe Biden alimteuwa  kuwa mwakilishi maalumu wa masuala ya kibinadamu katika Mashariki ya Kati, hasa Gaza, atajiuzulu katika wiki za kadhaa zijazo. Kwa kuzingatia hali mbaya ya Gaza, hadi sasa haijulikani iwapo Biden atachagua mtu mwingine kuchukua nafasi ya Satterfield au la.

Kipindi cha Satterfield katika nafasi yake ya sasa kimekuwa na utata mwingi. Afisa huuyo wa serikakli ya Biden ndiye aliyetaka kuhamishwa wakimbizi wa Wapalestina kutoka Gaza na kupelekwa Misri. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Biden ilidai kidhahiri tu kwamba inapinga jambo hilo. Pendekezo hilo pia lilipingwa vikali na Wapalestina wenyewe na waungaji mkono wao. Pendekezo la kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi Misri linatia wasiwasi hasa ikizingatiwa kwamba linakumbusha tukio chungu la kulazimishwa Wapalestina kuyahama makazi yao katika mchakato uliojulikana kwa jina la "Nakbat". Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanakiangalia kipindi cha utendaji wa Satterfield kwa jicho la shaka na kueleza kuwa, katika kipindi cha uongozi wake, hali ya wakazi wa Gaza iliambatana na misukosuko mingi na kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa eneo hilo la Palestina. Satterfield alipuuza hata wito wa mashirika ya misaada ya kibinadamu wa kufanyika vikao kwa ajili ya kuongezwa misaada ya wakazi wa Gaza.

Wakati huo huo, Satterfield anaondoka katika utawala wa Biden huku Washington ikiendelezahimaya yake kwa mashambulizi ya utawala haramu wa Israel huko Gaza. Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema kwamba Gaza inakabiliwa na njaa isiyo na kifani, na kwamba kiwango cha misaada ya kibinadamu inayotumwa katika eneo hilo ni duni sana kutokana na vikwazo vya utawala wa Kizayuni na Misri katika uwanja huo.

Kwa upande mwingine, sisitizo la viongozi wa utawala wa Kizayuni hususan Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu na mawaziri wenye misimamo mikali ndani ya serikali yake, la kuendeleza vita vya Gaza, ambavyo vimesababisha mauaji ya halaiki na kulazimisha zaidi ya asilimia 90 ya watu wa Gaza kuyahama makazi yao,  pamoja na maandamano makubwa ya kimataifa, sambamba na mashtaka yaliyowasiliswa na  Afrika Kusini dhidi ya Israel  katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, vimeifanya serikali ya Biden  ikabiliwe na matatizo mengi. Suala hilo limekuwa nyeti na zito kiasi kwamba limeweka wazi hitilafu za mitazamo kati ya Washington na Tel Aviv. Tovuti ya habari ya Axios imeandika katika ripoti yake kwamba ziara ya hivi majuzi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, huko  Palestina inayokaliwa kwa mabavu ilizidisha hali ya kutoridhia Ikulu ya White House kutokana na sera za kuendeleza hujuma na mashambulizi huko Gaza. Blinken alimweleza wazi Netanyahu kwamba mpango wake huko Gaza ni ndoto ambayo haitatimia. Gazeti la Kizayuni la Yediot Aharonot pia limeandika katika ripoti yake kwamba maafisa wa karibu wa Rais Joe Biden wa Marekani wanaamini kuwa Netanyahu anarefusha vita vya Gaza kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa. Netanyahu alisisitiza Jumamosi iliyopita kwamba hakuna anayeweza kuizuia Israel kuendeleza vita huko Gaza. Amedai kuwa ataendelea kukabiliana na Hamas na kurudisha eti amani katika mipaka ya kaskazini na kusini.