Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

19 Januari 2024

15:58:11
1430591

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran kushiriki mkutano wa NAM Uganda

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kwenda Kampala, mji mkuu wa Uganda kuhudhuria Mkutano wa 19 wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).

Shirika la habari la Iran Press liliripoti habari hiyo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran anatazamiwa kutoa hotuba muhimu katika mkutano huo wa NAM unaomalizika Januari 23.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iran anatazamiwa kuubanishia mkutano huo misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa. Kadhalika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa nchi mbalimbali kwenye mkutano huo wa kimataifa jijini Kampala.

Mkutano  huowa 19 wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) utashuhudia makabidhiano ya uongozi, ambapo mwenyeji Uganda inatazamiwa kuchukua usukani kutoka Jamhuri ya Azerbaijan.

Viongozi na wajumbe zaidi ya 4,000 kutoka takriban mataifa 120 duniani wamekusanyika katika mji mkuu wa Uganda, Kampala kwa ajili ya Mkutano wa 19 wa wakuu wa NAM ulioanza Januari 15. Katika kikao cha awali cha mkutano huo wa Kampala, Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mnasour aliwataka wajumbe kujadili mgogoro kati ya Palestina na Israel, na kusema kuwa licha ya kuwa harakati hiyo inakumbana na changamoto nyingi, mgogoro huo wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) ni wa dharura zaidi. NAM ilianzishwa mwaka 1961 katika kilele cha Vita Baridi kati ya Magharibi na Mashariki. Lakini, tofauti na mashirika mengine ya kikanda na kimataifa, haina mkataba rasmi wala sekretarieti ya kudumu. Nchi yenye uenyekiti wa mzunguko ina jukumu la kuratibu na kusimamia mambo ya jumuiya.

342/