Main Title

source : Parstoday
Jumapili

21 Januari 2024

15:56:29
1431269

Shambulio la kigaidi la Israel dhidi ya Syria na kuuawa shahidi washauri watano wa Iran

Washauri watano wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliuawa shahidi jana Jumamosi katika shambulizi la kigaidi la anga lililofanywa na utawala wa Kizayuni huko Damascus, mji mkuu wa Syria.

Ni mara kadhaa sasa katika wiki za karibuni utawala wa Kizayuni unafanya shambulio la kigaidi katika maeneo tofauti ya Syria na Lebanon kwa lengo la kusimamisha wimbi jipya la mapambano ya kupigania haki ya Muqawama wa Palestina na Lebanon dhidi ya utawala huo ghasibu. Mbali na kutokuwa na uhalali wa kisheria mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Wazayuni dhidi ya viongozi wa muqawama wa Lebanon na Palestina pamoja na washauri wa kijeshi wa Iran katika nchi za Syria, Lebanon na Iraq, kimya cha kutisha kilichoonyeshwa na waungaji mkono wao wa Magharibi kwa vitendo hivyo vya kigaidi vya Wazayuni hao wenye kiu ya damu, ni ishara nyingine ya wazi kabisa ya uungaji mkono na ushirikiano wenye maana maalumu unaoonyeshwa na Magharibi kwa jinai hizo. Katika taarifa ambayo liliitoa jana hiyohiyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza kuwa, washauri wake watano wa kijeshi, walinzi wa haram tukufu na askari kadhaa wa jeshi la Syria wameuawa shahidi, kufuatia jinai ya kinyama iliyofanywa jana mchana na utawala wa Kizayuni kwenye eneo la Al-Mazzah katika mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Kabla ya hapo na katika wiki za karibuni pia, Sayyid Razi Mousavi, mmoja wa washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria, Wassam At-T'awil mmoja wa makamanda wa Hizbullah nchini Lebanon na Saleh Al Arouri, Naibu Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS waliuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na utawala katili wa Kizayuni huko Syria na Lebanon. Abu-Taqawi As-Saeidi, mmoja wa makamanda wa harakati ya An-Nujabaa ya Iraq, yeye aliuawa shahidi mwezi uliopita katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani huko Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Ingawa lengo la Wazayuni la kuwaua maafisa na makamanda wa muqawama na washauri wa kijeshi wa Iran katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita limetajwa kuwa ni kusimamisha harakati za mhimili wa muqawama na kudhoofisha ari ya wapiganaji wa mhimili huo, lakini mapambano ya kwenye medani za vita katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita yamethibitisha kuwa, baada ya kila shambulizi la kigaidi la utawala huo, wigo wa mapambano dhidi ya Uzayuni umepanuka na kuenea zaidi katika medani tofauti, na kuanzishwa medani mpya ya mashambulio dhidi ya utawala huo haramu katika eneo. Kujiunga vikosi vya Ansarullah ya Yemen na vya Muqawama wa Iraq kwenye medani ya vita na mapambano dhidi ya wanajeshi wa Kizayuni na Marekani kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu na waliozingirwa wa Gaza ni ushahidi tosha wa kuthibitisha ukweli huo. 

 342/