Main Title

source : Parstoday
Jumanne

23 Januari 2024

14:42:47
1431829

Palestina: Kwa siku 108, Israel imeua watoto 11,000 na wanawake 7,500 Gaza

Mamlaka za Palestina zimetangaza kuwa, jeshi vamizi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeua watoto 11,000 na wanawake 7,500 katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa jeshi hilo katili limedondosha zaidi ya tani 65,000 za mada za miripuko katika vita vya upande mmoja lilivyoanzisha dhidi ya Wapalestina waliowekewa mzingiro.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatatu imeendelea kueleza kuwa, Wapalestina wapatao 7,000 - asilimia 70 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto - bado wako chini ya vifusi au wamepotea kutokana na mashambulizi ya kiholela ya jeshi la Israel.

Takwimu zinazoakisi ukubwa wa jinai na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni katika Ukanda wa Gaza zinaonyesha pia kwamba, mashambulio ya jeshi hilo yamebomoa kikamilifu nyumba zipatazo 70,000 na kuzifanya zingine 290,000 zisiweze kukalika kutokana na vita vyake vya siku 108 dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.

Kuhusu mashambulizi ya jeshi la Kizayuni kwenye sekta ya afya, Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Gaza zimeeleza kuwa jeshi hilo hadi sasa limeshawaua wafanyakazi 337 wa kada ya afya na tiba na maafisa 45 wa ulinzi wa raia.

Halikadhalika, tangu Oktoba 7, 2023 jumla ya waandishi wa habari 119 wameuawa katika mashambulizi ya kiholela yaliyofanywa na jeshi la Israel.Ikiashiria hali mbaya ya kibinadamu inayotawala katika makazi yenye msongamano wa watu ambapo Wapalestina waliokimbia makazi yao wanatafuta hifadhi, taarifa ya Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Gaza imesema, kesi 400,000 za maradhi ya kuambukiza na zaidi ya nyingine 8,000 za Homa ya Ini zimegunduliwa kutokana na athari za uvamizi wa Israel na kuhama kwa watu wengi. Sambamba na hayo, wanawake 60,000 wajawazito huko Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa ya kushindwa kujifungua salama kutokana na kukosekana huduma za afya, wakati watu wengine 350,000 wenye maradhi sugu wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa dawa. Jeshi la utawala wa Kizayuni limebomoa kikamilifu majengo 140 ya serikali pamoja na skuli na vyuo vikuu 99, mbali na kuharibu pia vyuo vikuu 295. Nje ya Ukanda wa Gaza, kuna majeruhi 11,000 wanaohitaji matibabu, na wagonjwa 10,000 wa saratani ambao wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na huduma duni za afya. Ripoti ya Mamlaka za Palestina Gaza imeongeza kuwa jeshi la Kizayuni limebomoa misikiti 253 na kusababisha uharibifu kwa makanisa matatu ya eneo hilo. Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, Wapalestina wasiopungua 25,900 wameuawa shahidi na wengine 63,000 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na jeshi la Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza.../

342/