Main Title

source : Parstoday
Jumanne

23 Januari 2024

14:43:24
1431830

Axios: Israel imependekeza kwa HAMAS mpango mpya wa kubadilishana mateka

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umependekeza kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS mpango mpya wa kubadilishana mateka kupitia "usitishaji" mapigano kwa muda wa hadi siku 60 ili mateka wote waliosalia, ambao wanashikiliwa na harakati hiyo, waweze kuachiwa.

Maafisa wawili wa utawala wa Kizayuni ambao hawakutajwa majina yao wamemueleza ripota wa tovuti ya habari ya Axios Barak Ravid kwamba, baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni lilishaidhinisha nukta kuu za pendekezo hilo tangu siku kumi zilizopita na kuzituma kwa Hamas kupitia Qatar na Misri.

Kwa mujibu wa Axios, utawala haramu wa Israel sasa unasubiri majibu ya harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina.Tovuti ya Axios imeeleza kuwa, chini ya masharti ya pendekezo hilo la Israel, awamu ya kwanza ya kubadilishana mateka itashuhudia Hamas ikiwaachilia wanawake, wanaume wenye umri zaidi ya miaka 60, na mateka wenye hali mbaya sana za kiafya. Awamu ya pili itahusisha kuwaachilia askari wa kike, raia wa kiume wenye umri chini ya miaka 60, wanajeshi wanaume, na hatimaye miili ya mateka waliouawa. Kwa mujibu wa maafisa hao wa Kizayuni, Israel iko tayari kusitisha operesheni za mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Gaza kwa muda wa "hadi miezi miwili," ambao utakuwa muda mrefu zaidi tangu waziri mkuu wa utawala huo wa Kizayuni Benjamin Netanyahu atangaze kile alichokiita vita dhidi ya Hamas. Hata hivyo, kulingana na pendekezo hilo, utawala huo hauko tayari kukomesha vita kikamilifu au kuwaachilia mateka wote 6,000 wa Kipalestina unaowashikilia kidhulma kwenye magereza yake. Kulingana na pendekezo hilo, Hamas na utawala wa Kizayuni zitapaswa kukubaliana mapema ni mateka wangapi Wapalestina wataachiliwa huru kwa kila Muisraeli katika kila kundi la mateka wa Kizayuni, na kujadiliana pia kuhusu majina ya mateka hao wa Kipalestina. Pendekezo hilo linajumuisha pia "kuondolewa" jeshi la Kizayuni katika baadhi ya sehemu za Gaza na kuruhusu "kurudi polepole" Wapalestina kwenye eneo hilo. Iwapo harakati ya Hamas itaukubali mpango huo uliopendekezwa na Israel, operesheni za jeshi la utawala huo wa Kizayuni huko Gaza zitaendelea baada ya siku 60 lakini zitakuwa "ndogo sana kwa upande wa wigo na nguvu zake".../

342/