Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

25 Januari 2024

13:33:46
1432353

Ansarullah yaitaka UN iwaondoe Yemen wafanyakazi wake raia wa US, UK

Harakati ya Ansarullah imeziagiza Marekani na Uingereza ziwaondoea nchini Yemen raia wake wanaoufanyia kazi Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu, Sana'a.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imetoa amri hiyo katika barua iliyomuandikia Peter Hawkins, Kaimu Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen. 

Sehemu moja ya barua hiyo ya Ansarullah kwa UN inasema, "Wizara inapenda kusisitiza kuwa, lazima muwataarifu maafisa na wafanyekazi wenu raia wa Marekani na Uingereza wajiandae kuondoka nchini (Yemen) katika kipindi cha siku 30."

Aidha barua hiyo imeyaagiza mashirika ya kigeni yanayofanya kazi ya kusambaza misaada ya kibinadamu nchini Yemen yasiwaajiri raia wa Marekani na Uingereza.

Wakati huo huo, Mohammed Abdulsalam, Msemaji wa Ansarullah amelithibitishia shirika la habari la Reuters kuhusu uhalali wa barua hiyo ya kuzitaka Marekani na Uingereza ziwaondoea nchini Yemen raia wake wafanyakazi Umoja wa Mataifa.

Haya yanajiri wakati huu ambapo hali ya usalama katika Bahari Nyekundu imezidi kuwa mbaya kufuatia mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Wayemen katika siku za hivi karibuni. 

Harakati ya Ansarullah ya Yemen ilianza kushambulia meli za kijeshi za Marekani na Uingereza baada ya nchi hizo mbili kuingilia kati kwa ajili ya kulinda meli za mizigo za utawala haramu wa Israel zinazoshambuliwa na Wayemen kwa lengo la kuulazimisha utawala huo usitishe mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina. 

Ansarullah imesema kuwa, meli nyingine zote isipokuwa za Marekani, Uingereza na Israel zipo salama kupita katika maji ya Bahari Nyekundu na kusisitiza kuwa, hazitalengwa na kushambuliwa na vikosi vya Yemen. Jeshi wa la Yemen limesema vikosi vyake vitaendelea kujibu uvamizi na uchokozi wa Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen kupitia mashambulizi ya ardhini na baharini.

342/