Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Januari 2024

17:46:45
1433239

Biden ashtakiwa Marekani kwa "kushiriki" mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel Gaza

Mahakama moja ya mji wa Oakland katika jimbo la California, imesikiliza mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya Rais wa Marekani Joe Biden na maafisa kadhaa waandamizi wa nchi hiyo ya "kushiriki katika mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel Gaza".

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi sasa, utawala wa Kizayuni unafanya mashambulizi makubwa na ya kinyama katika Ukanda wa Gaza ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 26,000 na wengine zaidi ya 64,000 kujeruhiwa; na mashambulizi hayo yangali yanaendelea licha ya kupingwa na kulaaniwa kimataifa. Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, mahakama ya serikali ya shirikisho katika mji wa Oakland, California, imesikiliza mashtaka yaliyofunguliwa na Kituo cha Haki za Kikatiba, Center for Constitutional Rights (CCR) kikiwakilisha makundi kadhaa ya haki za binadamu ya Palestina, wakazi wa Gaza, na raia wa Marekani ambao jamaa zao wameathirika kutokana na mashambulio ya mtawalia ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ukanda wa Gaza.Katika madai yao, washtaki hao wamesema, maafisa wa serikali ya rais Joe Biden hawajazuia mauaji ya kimbari ya wananchi wa Palestina huko Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Katika mahakama hiyo, rais wa Marekani Joe Biden, waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken na waziri wa ulinzi Lloyd Austin wameshutumiwa kwa "kushindwa kuzuia vitendo vya Israel na kushiriki katika mauaji ya wazi kabisa ya kimbari".

 Mashtaka ya Kituo cha Haki za Kikatiba, yaliwasilishwa kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2023 ambapo ilitangazwa kwamba Biden, Blinken na Austin "sio tu wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuzuia mauaji ya kimbari, lakini pia wameandaa mazingira ya kushamirishwa na kushadidishwa kwa kutoa bila masharti yoyote misaada ya kijeshi na kidiplomasia kwa Israel. Katika kesi hiyo, Kituo cha Haki za Kikatiba kinaiomba mahakama kutangaza kwamba, "washtakiwa wamekiuka wajibu wao chini ya sheria zinazokubalika kimataifa kuizuia Israel kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza." Kituo hicho pia kinaitaka serikali ya Marekani kutumia ushawishi wake kwa utawala wa Kizayuni ili kukomesha uadui wake dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Ripota wa Al Jazeera, Rob Reynolds ameripoti kutoka mahakama hiyo ya Oakland kwamba CCR imesema Marekani inakiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948 kwa kutuma silaha kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel. Mkataba huo umeyatafsiri mauaji ya kimbari kama hatua yoyote inayolenga kuteketeza kikamilifu au kwa kiwango fulani taifa, rangi, kabila au dini.../


342/