Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

29 Januari 2024

14:20:30
1433495

Kushitakiwa Biden katika mahakama ya California kwa kuunga mkono mauaji ya kimbari

Sambamba na kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza na sambamba na hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ya kutoa hukumu dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa jinai zake hizo, hivi sasa wimbi la kulaani jinai za Wazayuni na waungaji mkono wake nalo linazidi kuwa kubwa, siku baada ya siku.

Taasisi na Wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu huko Palestina wamefungua kesi katika mji wa Auckland wa jimbo la California kuishitaki serikali ya Marekani na Joe Biden mwenyewe kutokana na kushhindwa kuzuia mauaji ya kizazi wanavyofanyiwa Wapalesina wa Ghaza.

Walioshitakiwa kwenye kesi hiyo ni rais wa Marekani, Joe Biden, waziri wa mambo ya nje, Antony Blinken, na waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd James Austin, kutokana na kushiriki kwao moja kwa moja kwenye mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

Kwa kweli tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya wananchi wa Ghaza tarehe 7 Oktoba, Marekani ndiyo iliyochukua nafasi ya juu zaidi ya kuunga mkono jinai hizo; kisilaha, kisiasa, kipropaganda na kwa kila kitu. Viongozi wa Marekani wamekuwa wakipigana vikumbo huko Israel na kila mmoja anajaribu kuthibitisha kivitendo uungaji mkono kamili wa Washington kwa jinai za utawala wa Kizayuni. Safari ya karibuni kabisa ni ile iliyofanywa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken aliyeutembelea utawala wa Kizayuni ili kuzuia kusimamishwa vita huko Ghaza.Vilevile katika kipindi cha miezi minne iliyopita, serikali ya Marekani imetumia mamilioni ya dola kuisheneneza silaha Israel ili izidi kufanya mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina. Hadi hivi sasa Marekani imeshaupa utawala wa Kizayuni silaha za kubebwa na ndege 230 na meli 20 za mizigo. 

Katika kipindi cha siku chache nyuma na licha ya kuweko mashinikizo ya kila upande ya kimataifa ya kulaani jinai za Israel na hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ ya kupinga jinai hizo, lakini viongozi wa Marekani wametangaza habari ya kuupelekea utawala wa Kizayuni shehena nyingine ya silaha ambayo ndani yake mna makumi ya ndege za kivita za F35 na helikopta 15 aina ya Apachi. 

Uungaji mkono huo wa waziwazi kabisa wa serikali ya Biden kwa jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, umewalazimisha hata waitifaki wa karibu wa Marekani kutangaza hadharani kwamba wanapinga vikali uungaji mkono huo wa kibubusa. Upinzani huo mkubwa unashuhudiwa hata ndani ya Baraza la Congress la Marekani kwenyewe. 

Seneta Bernie Sanders anasema: Kila mwaka Marekani inaipa Israel msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8. Hivi sasa pia, mabomu na zana zote zinazotumiwa na Israel kuiteketeza Ghaza; zote zimetengenezwa Marekani. Kwa maneno mengine ni kwamba, sisi Marekani ni washiriki wa matukio yanayoendelea hivi sasa huko Ghaza na kwamba mambo yanayotokea huko hivi sasa hakuna ulimi unaoweza kuyabainisha ipasavyo.